
Mhandisi Robert Kitundu ameanza kazi rasmi kama Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT, akichukua nafasi ya ndugu Brighton Kilewa ambaye amestaafu.
Akizungumza wakati wa kumtambulisha Katibu Mkuu huyo mpya kwenye Ofisi za Makao Makuu ya KKKT yaliopo Arusha, Mkuu wa KKKT na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Mch Dkt. Fredrick O. Shoo amemtaka Katibu Mkuu huyo kufanya kazi kwa nguvu na kwa uaminifu akishirikiana na watendakazi wa Ofisi Kuu ya KKKT ili kuendelea kulijenga Kanisa la Mungu.
Katibu Mkuu huyo wa KKKT, Mhandisi Robert Kitundu amelishukuru Kanisa kwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa uaminifu na ushirikiano ili kutimiza kusudi la Mungu.
Akizungumza kwa niaba ya watendakazi wa Ofisi Kuu ya KKKT, Naibu Katibu Mkuu Huduma za Jamii, Wanawake na Watoto Mch. Rachel Axwesso amesema kuwa watendakazi wa Ofisi Kuu watampa ushirikiano Katibu Mkuu mpya katika utendajikazi wake na kuhakikisha kuwa shughuli zote za Ofisi Kuu zinatimizwa inavyotakiwa.
Katibu Mkuu Mstaafu wa KKKT, ndugu Brighton Killewa anastaafu huku akiwa amelitumikia Kanisa kwa muda wa miaka 16 katika nafasi ya Katibu Mkuu wa KKKT tangu alipoingia kazini mwaka 2005.

