Ikumbukwe kuwa kupitia Halmashauri Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazani Mashariki kwa kauli moja ilipitisha mwaka 2022 uwe mwaka wa Wanawake katika Dayosisi huku ukiongozwa na kauli mbiu kutoka kitabu cha Waamuzi 5:12a: - Amka ,Amka ,Debora; Amka,amka, imba wimbo.
Wanawake wa Usharika huo wamemshukuru kipekee Baba Askofu kwa kuacha shughuli zake na kuungana nao katika kuadhimisha siku ya kongamano la wanawake katika Usharika huo.
“Ndugu mgeni rasmi tunaishukuru Dayosisi yetu kuufanya mwaka 2022 kuwa mwaka wa Wanawake kidayosisi, kwani imetusaidia kufahamiana, kushirikiana kutatua changamoto mbalimbali, kutiana moyo kuinuana kiroho pale ambapo tumekata tamaa na kiuchumi”.
Wanawake wa Usharika wa Irente, katika kutimiza malengo mbalimbali waliyojiwekea katika mwaka huu wamefanikiwa kutekeleza mambo yafuatayo :
Kwanza kufanya uzinduzi wa mwaka wa Wanawake kiusharika, kufanya semina ya Wanawake iliyohusu wajibu wa Mwanamke katika Kanisa na jamii kwa ujumla, kuimarisha na kuendeleza kikundi cha VICOBA cha Wanawake usharikani.
Kuendeleza kazi za mikono za Wanawake usharikani na katika jumuiya ambazo ni kama ifuatavyo Mradi wa Nguruwe, Mradi wa batiki, utengenezaji wa kapeti,ususi wa mikeka na vikapu, utengenezaji wa sabuni, usimamiaji sikukuu za mikaeli na Watoto, maombi ya dunia na maandalizi ya Ibada ya Advent.
Wanawake wa Usharika wa irente pia wameweka alama ya utengenezaji wa Mabenchi 10 (kumi) ya kukalia kama uwekaji wa alama ya kumbukumbu yao ya maadhimisho ya mwaka wa wanawake 2022. Ambapo leo walikabidhi mabenchi matatu (3) ambayo yapo tayari kutumika huku wakikabidhi payslip ambayo fedha yake imekwisha ingizwa benki kiasi cha Tshs. 100,000 (laki moja tu) kwa ajili ya mchango wao kukabiliana na deni la Dayosisi.Wameeleza kuwa wanafanya hivyo kuonyesha ni kiasi gani wanaguswa na shida viongozi wao wanayoipata kwa sababu ya madeni makubwa waliyorithishwa toka uongozi uliopita.