Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Dkt Msafiri Joseph Mbilu amewaomba wana KKKT-DKMs kumkumbuka katika sala na kumpa ushirikiano Katibu Mkuu mpya wa Dayosisi iliaweze kutekeleza majukumu yake vema.

“Ninawaomba ninyi wote tumuombee Katibu Mkuu huyu na kumpatia ushirikiano unaopasa ili aweze kutekeleza majukumu yake vema.”

Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo leo tarehe 20/11/2022 kwenye Ibada ya Jumapili iliyofanyika Kanisa Kuu Lushoto iliyoambatana na tendo la kumtambulisha rasmi Katibu Mkuu mpya wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mwl. Julius Samweli Madiga.

Askofu Dkt. Mbilu aliongeza kuwa Halmashauri Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki iliyoketi tarehe 9-10/12/2021 ilimuidhinisha Mch. Godfrey T. Walalaze kuwa Katibu Mkuu kwa muda wa Mwaka mmoja na kwamba baada ya Mwaka huo kukamilika apatikane Katibu Mkuu mpya.

Halmashauri Kuu iliyoketi tarehe 04/11/2022 kwa kauli moja ilipitisha jina la Mwl. Julius Samweli Madiga kuwa ndiye Katibu Mkuu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Masharki kuanzia tarehe 15/11/2022.

Mara baada ya kutambulishwa kwa wana KKKT-DKMs ,  Katibu Mkuu huyo mpya amesema kuwa amepokea wajibu huo kwa unyenyekevu mkubwa na kuwaomba wanadayosisi waliopo ndani na nje ya Dayosisi kumuombea kwa Mungu ili atimize vema wajibu alioitiwa.

KATIBU MKUU KKKT-DKMs MWL.JULIUS SAMWELI MADIGA 

Neno Kuu la Dayosisi yetu kutoka kitabu cha Zaburi ya 32:8 litaendela kuniongoza, nipo tayari kuitenda kazi hii niliyoitiwa nazidi kusisitiza washarika wenzangu waniombee na wanipe ushirikiano wa kutosha nitakuwa msikivu na nipotayari kuwatumikia wana KKKT-DKMs”.

Majina ya waliowahi kuwa Makatibu Wakuu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki pamoja na vipindi walivyotumika ni Kama ifuatavyo:1) Bw. Eliezer Mahimbo: 1969-1980. 2) Mch. Timilai Guga: 1980-1981. 3) Dkt. Gideon E. Chaguza: 1981-1986. 4) Bw. Fredrick Shebila: 1988-1999. 5) Mch. Godfrey Hermann: 2000-2003. 6) Mch. Jonathan Michael Mwamboza 2003-2006 7) Bw. Salatiel Shemhilu: 2006-2008. 8) Mch. James Mwinuka: 2008-2020. pamoja na Mch Godfrey Tahona Walalaze 2021-2022.

Miongoni mwa hawa, walio hai ni Mch. Godfrey Hermann, Mch. Jonathan Michael Mwamboza, Mch. James Mwinuka pamoja na Mch. Godfrey Tahona Walalaze.