Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amechukuwa hatua ya kuwaandikia barua washarika waliopo ndani ya Dayosisi juu ya ombi la mchango kwaajili ya kukabiliana na deni la Dayosisi.

Akizungumza leo tarehe 10/04/2022 katika Ibada ya Jumapili iliyo ambatana na uzinduzi wa uchangiaji wa deni hilo katika Usharika wa Kana Tanga, amewashukuru wana Dayosisi kwa jinsi wanavyojitoa katika kumtumikia Mungu na kujitoa kwao kwa hali na mali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili Dayosisi.

 

Mkuu wa Jimbo la Pwani, Mch. Thadeus A. Ketto

Askofu Dkt. Mbilu anachukua hatua hii kutokana na Dayosisi kudaiwa madeni makubwa na miongoni mwa madeni hayo ni hatarishi sana kwani yanaweza kusababisha mali za Dayosisi mfano Majengo, Mashamba, Magari nk. kupigwa mnada ili kufidia gharama za wale wanaoidai Dayosisi. Ofisi ya Katibu Mkuu imeanza kupokea taarifa za awali juu ya hatua hizo juu ya mali za Dayosisi kupigwa mnada.

Mkurugenzi wa fedha na Utawala KKKT-DKMs CPA. PETER JOHN SINGANI

Kwa ujumla deni la Dayosisi lililorithiwa toka Uongozi uliopita ni takribani Tsh. 7,000,000,000 (Bilioni Saba) likiwepo deni la mkopo wa CRDB, Mishahara na stahiki za watumishi wengine katika vituo mbalimbali vya Dayosisi kama vile Ofisi Kuu, SEKOMU, pamoja na madeni ya Mifuko ya kijamii kama vile NSSF, PSSSF pamoja na kodi mbalimbali.

Kwa kupitia sadaka ya maendeleo ya KKKT-DKMs imeendelea kupunguza baadhi ya madeni hayo kama vile deni la CRDB na sasa limeshuka kutoka Tsh. 1,200,000,000 (Bilioni Moja na nukta 2) hadi kufika Tsh.792,000,000 (Milioni Mia saba na Tisini na Mbili). Na hapa Askofu Dkt. Mbilu anamshukuru Mkuu wa Jimbo la Pwani Mch. Thadeus A. Ketto, Washarika wa Kana na wana Dayosisi kwa ujumla   kwa jinsi wanavyoendelea kujitoa katika utoaji wa sadaka hiyo.

Hata hivyo ili kuweza kukabiliana na madeni hayo makubwa, Askofu Dkt. Mbilu analeta ombi kwa washarika kwani wao ni kiungo muhimu cha Dayosisi hii kuchangia deni hilo kama viwango vilivyo ainishwa kwenye barua walizo pokea kwa kadri Bwana atakavyowajalia. Na hapa anawaomba wana Dayosisi katika awamu hii ya kwanza kuanza kuchangia sehemu ya deni hilo katika kipindi cha miezi sita yaani kuanzia tarehe 01/04 hadi tarehe 31/10/ 2022.

Ili kuweza kuhakikisha kuwa fedha hizi zinafika mahali sahihi, kwa wana Dayosisi waliopo ndani ya Dayosisi wanaombwa kuingiza fedha hizo moja kwa moja kwenye akaunti ya Dayosisi ambayo ni: -

  • NMB HARAMBEE ACCOUNT No. 41610027028 au
  • CRDB ELCT NORTH EASTERN DIOCESE Acc.No.01J1029661501

Askofu Dkt. Mbilu ametanabaisha kuwa hatua ya pili ya uchangiaji kwa wadau wa maendeleo na wana KKKT-DKMs waliopo nje ya Dayosisi utatangazwa hivi karibuni. Uongozi unakutakia baraka za Mungu katika Utumishi wako shambani mwa Bwana.