Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amesema uongozi wa Dayosisi unatambua mchango mkubwa wa walimu pamoja na watumishi waliopewa dhamana ya kutumika katika Taasisi za Elimu ndani ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.
 
Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo leo tarehe 13/03/2025 akiwa kwenye ziara yake ya kikazi katika Shule ya Sekondari Lwandai inayomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na kuongeza kuwa ameona ni vema kufika shuleni hapo kuonana na Walimu,wafanyakazi wengine pamoja na wanafunzi wa shule hiyo kwa lengo moja la kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa pamoja iliyopelekea ufaulu mzuri wa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne 2024.
 
Pamoja na pongeza hizo Askofu Dkt. Mbilu ametoa mkono wa pongezi kwa Walimu pamoja na watumishi wote ikiwa ni ishara ya kutambua na kuthamini kazi kubwa inayofanyika Shuleni hapo.
Askofu Dkt. Mbilu ameongeza kwa kusema kuwa sasa shule zinazomilikiwa na KKKT-DKMs zinatambulishika mbele za watu huku akiwataka walimu pamoja na wafanyakazi wa Shule hiyo kuendeleza ushirikiano na mshikamano kati yao ili kuongeza ufaulu zaidi huku wakihakikisha suala la maadili linapewa kipaumbele.
 
Pamoja na hayo Baba Askofu Dkt. Mbilu, ametimiza ahadi yake aliyoitoa kwenye mahafali ya 35 ya kidato cha nne yaliyofanyika tarehe 19/10/2024 ambapo aliahidi kutoa tarumbeta na leo ametimiza ahadi hiyo kwa kukabidhi tarumbeta ndogo moja na baada ya kusikiliza upigaji sahihi wa tarumbeta kutoka kwa darasa la tarumbeta la Shule hiyo ametoa ahadi ya kuongeza tarumbeta nyingine.Darasa la tarumbeta katika Shule ya Sekondari Lwandai kwa sasa lina jumla ya wanafunzi wa muziki 25.
 
Tufuatilie kwenye mitandao yetu ya kijamii
INSTAGRAM - / elctned
FACEBOOK ACCOUNT North Eastern Diocese
FACEBOOK PAGE - ELCT-North Eastern Diocese
YOUTUBE - / KKKT DKMS Online TV
KWA MAONI NA USHAURI:
Simu : +255 743 399 798