KATIKA PICHA:Mazishi ya Mama Askofu Elfriede Sebastian Kolowa iliyofanyika KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,Usharika wa Kanisa Kuu Lushoto leo tarehe 06/03/2025. Ibada hii iliongozwa na Mkuu wa KKKT Baba Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa.Marehemu, Bibi Elfriede Sebastian Kolowa alizaliwa tarehe 30 mwezi Juni mwaka 1934 huko Bumbuli Salem Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga akiwa Mtoto wa 6 wa Mwalimu Emmanuel Chamshama na Bibi Sarah Shemshi.Mwili mwili wake umepumzishwa leo tarehe 06/03/2025 katika makaburi yaliyopo katika eneo la Kanisa Kuu Lushoto.Sehemu ya historia ya Bibi Elfriede Sebastian Kolowa inaeleza kuwa.
Kuzaliwa
Bibi Elifriede Sebastian Kolowa alizaliwa tarehe 30 mwezi wa June mwaka 1934 huko Bumbuli, Salem Wilaya ya Lushoto, Mkoa wa Tanga, akiwa ni mtoto wa 6 wa Mwalimu Emmanuel Chamshama na Bibi Sarah Shemshi. Alibatizwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Usambara Digo Usharika wa Bumbuli mnamo tarehe 16 Oktoba, 1934 wadhamini wake wa ubatizo walikuwa ni Mwalimu Tadeo Kwalazi na Bibi Zipora Kwalazi.
Elimu
Bibi Elifriede Kolowa alipata elimu katika shule ya msingi Bumbuli toka darasa la 1 mpaka alipomaliza elimu yake akiwa darasa la 6. Aliingia shule mwaka 1942 - 1948.
Alipata kipaimara tarehe 25 Desemba 1950 katika Usharika wa Bumbuli, siku ya mashangilio ya kuzaliwa kwa mkombozi wa wanadamu yaani Yesu Kristo. Bibi. Elfriede aliwahi kuwa mwalimu wa Shule ya Jumapili (Sunday School) kwa muda wa miaka 6, yaani kuanzia mwaka 1951 - 1956. Aliwahi pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Vijana wa Kikristo katika Usharika wa Bumbuli. Wakati huo Mwenyekiti alikuwa Kundaeli Kwalazi.
Ndoa
Bibi Elifriede Kolowa alifunga ndoa takatifu na Mwalimu Sebastian Ignatio Kolowa, tarehe 16 Desemba 1956 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Usambara/Digo katika Usharika wa Bumbuli. Katika ndoa yao, Mungu aliwabariki kupata watoto 4 na wajukuu 9. Ndoa yao ilifungwa Bumbuli na Mch. Gideon Kwalazi
Utumishi
Baada ya kufunga ndoa Bibi Elifriede Kolowa, aliambatana na mumewe kwenda kuishi Mbuzii - Soni wakati huo Mwalimu Sebastian Ignatio Kolowa ndiye aliyekuwa Headmaster wa Shule hiyo iliyokuwa Middle School, shule hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Usambara/Digo. Mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo alikuwa ni Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Mh. Yusufu Makamba. Mwaka 1960 – 1967 alikuwa Ujerumani na mume wake. Wakati huo Mwl. Sebastian Kolowa alikuwa akichukua mafunzo ya Shahada ya Uzamili ya Theologia katika Chuo Kikuu cha Hamburg nchini Ujerumani. Bibi Elfriede naye hakurudi nyuma alijifunza lugha ya Kijerumani, Kiingereza, Maarifa ya Nyumbani, Maisha ya mwanamke wa Kijerumani na maisha ya mwanamke wa Kitanzania.
Mwaka 1969 - 1972 Waliishi Vuga mume akiwa Mkuu wa Lutheran Junior Seminary kabla haijahamishiwa Morogoro ambapo kwa sasa inajulikana kama Lutheran Junior Seminary. Mwaka 1967 mwishoni alirudi nyumbani na Familia yake. Mwalimu Sebastian Kolowa akapangiwa kwenda Vuga kuwa Mkuu wa Shule ya Junior Seminary ambapo baadaye Shule hiyo ilihamishiwa Morogoro. Wakati aliporudi nyumbani tayari Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Usambara Digo lilikuwa limebadilisha jina na kujulikana kwa jina la KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki. Hiyo, ilitokana na kuundwa kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kulikofanyika mwaka 1963 ambapo Baba Askofu Stephano Reuben Moshi alichaguliwa kuwa Mkuu wa Kwanza wa KKKT. Baada ya muda mfupi Mwalimu Sebastian alibarikiwa kuwa Mchungaji, akawekwa kuwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Lushoto, wakati huohuo akiwa Katibu Mkuu. Bibi. Elfriede Kolowa aliendelea kulea familia, wakati mumewe akiwa Mch. Kiongozi, Katibu Mkuu na Msaidizi wa Askofu (Baba Dean). Na baadaye alichaguliwa kuwa Askofu wa DKMs, mwaka 1972.
Kwa takribani miaka 21 kuanzia mwaka 1976 - 1997, wakati huo Mwenyekiti wa Idara ya wanawake alikuwa Bibi Elizabeth Hermann wa Tanga na baadaye alipokelewa na Bibi Anna Kaniki wa Mlalo. Elifriede Kolowa alistaafu na kukabidhi wajibu huo kwa Mch. Joyce Kibanga. Tarehe 3 Jan, 1998 aliagwa rasmi na Ofisi Kuu katika tafrija iliyofanyika Utondolo - Lushoto. Tendo hilo lilifanyika na Kwaya Kuu ya Kanisa Kuu wakiwa wamevaa Kanga zilizoandikwa “Nani Kama Mama”. Katika kipindi chake cha uongozi alikuwa Mama mwenye bidii na utayari wa wakati wote. Wengi miongoni mwa wale waliofanya kazi wanathibitisha ukweli wa kujitoa kwake kwa kushirikiana na kila aliyefanya kazi naye bila ya ubaguzi wowote. Aliyekuwa Mwenyekiti wake wa Idara wakati huo alishirikiana naye kwa karibu na kuhakikisha akinamama wengi zaidi wananufaika na mazao ya kazi za idara badala ya yeye kujipendelea na kunufaika mwenyewe. Mama Anna Kaniki ndiye aliyekuwa Mwenyekiti miongoni mwa watu waliomshauri vizuri na kuipeleka idara ya wanawake mbele. Hata hivyo kati ya majina aliyokuwa nayo ni kubwa:
- Aliitwa BIBI MAENDELEO kwa sifa ya utendaji wake na utayari wa utumishi wake akiwashirikisha wengine.
- Aliitwa mama wa imani kwani alikaza sana na kuwataka watu KUOMBA kila wakati. Kwake maombi lilikuwa jambo la msingi katika utendaji wa kazi. Mama Kolowa alihimiza sana miradi ya ujasiriamali ili kukuza uchumi wa Familia. Aidha alikuwa kielelezo cha kazi na maisha ya ushuhuda. Ndani ya idara yake alitoa huduma za Diakonia kwa waliokuwa wahitaji - 25: 34 - 40.
Bibi Kolowa alimtunza vizuri mume wake na kumwezesha kujiwekea majukumu yake mengi na mazito ya KKKT ya kijamii na kimataifa. Alikuwa na moyo wa furaha wakati wote, upendo, utulivu na unyenyekevu na alikuwa na moyo wa kuipenda familia yake. Aidha alikuwa mkarimu mcheshi, mchangamfu na mtanashati. Alikuwa mjumbe wa Bodi ya mamlaka ya maji Wilaya ya Lushoto kuanzia terehe 12 Mei, 2008 hadi tarehe 12 Mei, 2011. Katika kipindi hicho cha miaka 3 Bibi. Elfriede alikuwa anawakilisha kundi la wanawake. Katika kipindi hicho cha miaka 3 Bibi. Elfriede Sebastian Kolowa alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Bwana William W. M. Kusaga - Mwenyekiti. Akiwa katika Bodi hiyo pamoja na wajumbe wengine na Menejimenti ya Maji Lushoto, walifanya ziara ya mafunzo ya siku mbili kwenye mamlaka ya maji safi na maji taka Moshi Kilimanjaro. Maeneo waliyotembelea ni;
- Ofisi za mamlaka ya maji safi na maji taka Moshi na vitengo vyake vyote vya Utendaji.
- Kutembelea chanzo cha maji kilichopo Nshiri. Tanki la maji Kilimanjaro na visima virefu vilivyopo KCMC.
- Kituo cha kuchotea maji kilichopo Kiboriloni, kilichofungwa mita ya maji ya pre-paid.
- Kutembelea eneo la Mabogini sehemu ambayo ni ya kusafisha maji taka.
- Kufanya kikao cha pamoja katika Bodi ya mamlaka ya maji Moshi na Bodi ya Lushoto.Ni katika kipindi hicho mamlaka ya maji Lushoto ilifanya kazi zake vema na kuwa na mafanikio makubwa. Mwaka 2015Mkuu wa Wilaya ya Lushoto alimteuwa Bibi Elfriede kuwa mjumbe wa Baraza la Wazee Lushoto.
Bibi Elifriede Kolowa ameugua kwa muda mpaka mauti ilipomfika. Miongoni mwa waliomhudumia kutokana na maradhi hayo ni wengi. Hata hivyo waliomhudumia katika kuugua kwake ni kweli kwamba ni wengi, lakini ukweli utabaki palepale kwamba amehudumiwa vizuri; kifo ni mpango wa Mungu, si kwake tu lakini kwa kila aitwaye mwanadamu. Madaktari toka hospitali zote ambazo Mama yetu, alihudumiwa iwe ni hapa Lushoto, Kule Dar es salaam na pengine popote. Tunawatakia neema na Baraka za Mungu. Tunaomba kwa ajili yao kwamba Baraka za Mungu, ziwatunze na kuwapa nguvu kwa upya ili waweze kuwahudumia na wengine walio katika hali ya uhitaji.