Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, anasikitika kutangaza kifo cha Mchungaji Mstaafu Daniel Magogo, kilichotokea tarehe 16/05/2024, nyumbani kwake Kwesimu Lushoto Tanga.

Marehemu Mchungaji Mstaafu Daniel Magogo katikauhai wake alishawahi kuwa Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (Church President) kati ya mwaka 1965-1970.

Ibada ya mazishi  itafanyika katika Usharika wa  Kanisa Kuu Lushoto siku ya Jumatatu ya tarehe 20/05/2024 saa 4:00 Asubuhi.Na mara baada ya Ibada mwili wa Marehemu Mchungaji Mstaafu Daniel Magogo utapumzishwa katika makaburi ya familia yaliyopo Kwesimu Lushoto Tanga.

Tunamshukuru Mungu kwa mema mengi tuliyopokea kutoka kwa Mtumishi wake huyu.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa Jina la Bwana na lihimidiwe.

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amesema anaimani na wakurugenzi wapya waliochaguliwa hivi karibuni kusimamia Kurugenzi mbalimbali za Dayosisi huku akiwataka waumini pamoja na wakuu wa vituo vya Dayosisi kuwapa ushirikiano ili waweze kutimiza malengo yanayokusudiwa.



Askofu Dkt. Mbilu, ameyasema hayo katika Ibada ya Jumapili ya tarehe 12/05/2024 iliyofanyika katika Jimbo la Tambarare Usharika wa Korogwe na kuongeza kuwa sasa Kurugenzi zote za Dayosisi zimekamilika kwakuwa na Wakurugenzi wenye sifa baada ya nafasi hizo kukaimiwa kwa kipindi kirefu, hivyo anaamini Wakurugenzi hao utendaji wao wa kazi utaleta matokeo chanya na manufaa kwa Dayosisi.

Wakurugenzi hao wapya ni Mkurugenzi wa Uchumi, Mipango na Maendeleo Bibi, Pendo Wilfred Lauwo na Mkurugenzi wa huduma za jamii Bw. Afizai Vuliva. Aidha Baba Askofu amemtambulisha Rasmi Mkuu wa Jimbo Mteule wa Jimbo la Tambarare Mch. John Ndimbo na hivyo kumtakia baraka za Mungu katika utendaji wake wa kazi huku akimtaka kuendeleza mambo mazuri aliyoyafanya mtangulizi wake Mch. Frank Mtangi. Mch. John Ndimbo amechukuwa nafasi ya kuliongoza Jimbo la Tambarare baada ya Mtangulizi wake Mch. Frank Mtangi kuhamishiwa Jimbo la Pwani.

Ibada hii iliyoambatana na matendo mbalimbali pia Washarika wa Usharika wa Korogwe waliitumia Ibada hiyo kuungana na Wanadayosisi kwa ujumla kumuombea na kumtakia heri na baraka Baba Askofu Dkt. Mbilu, kufuatia kufikisha miaka Mitatu (3) toka kuingizwa kazini.

Ikumbukwe kuwa Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, aliingizwa kazini katika Ibada iliyofanyika Kanisa Kuu Lushoto tarehe 09/05/2021, na kisha yeye kumuingiza kazini msaidizi wake, Mch. Michael Mlondakweli Kanju hivyo 09/05/2024 alitimiza miaka hiyo mitatu ya kuiongoza KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Mei 9 mwaka 2021 ilikuwa ni siku iliyotawaliwa na nderemo, vifijo na shamrashamra katika viunga vya Lushoto, siri nyuma ya furaha hii si nyingine bali ni historia mpya kuandikwa, wakristo wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki walipata Askofu mpya, kiongozi ambae atayabeba maono na dira ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki huyu sio mwingine bali ni Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu.

Baba Askofu Dkt. Mbilu, aliingizwa kazini katika Ibada iliyofanyika Kanisa Kuu Lushoto tarehe 09/05/2021, na kisha yeye kumuingiza kazini msaidizi wake, Mch. Michael Mlondakweli Kanju. sasa leo tarehe 09/05/2024 ni miaka mitatu ya Uongozi wa Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu tangu alipopewa kibali na Mungu cha kuiongoza KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.
 
Leo tarehe 09/05/2024 zimetimia siku 1,096, yaani miaka mitatu tangu alipoingizwa kazini kushika wadhifa huo , bado tunaiona shauku ileile ndani yake kwani licha ya kusimamia mafundisho sahihi ya Neno la , Askofu Dkt. Mbilu amesimamia msingi wa Dayosisi katika kumhudumia mwanadamu kimwili, kiakili na kiroho.

Askofu Dkt. Mbilu licha ya kusimamia Dayosisi kupitia kauli mbiu yake ya kasi tofauti, ameendelea kuwa mnyenyekevu na msikivu kwa washarika wote  kwani anaamini ushirikiano mzuri wanaompa ndio msingi wa mafaniko ya Dayosisi.

 
Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, pamoja na msaidizi wake Mch. Michael Kanju, wameshiriki kwenye uchaguzi wa kumpata Askofu Mpya wa Sinodi rafiki ya Southeastern Pennsylvania, iliyoko Philadelphia nchini Marekani , ambapo uchaguzi huo uliofanyika leo tarehe 05/05/2024 umekamilika na Mch. Bryan Penman amechaguliwa kuwa Askofu Mteule akichukuwa nafasi ya mtangulizi wake
 Askofu Dkt. Patricia Davenport aliyemaliza muda wake.

Katika uchaguzi huo Askofu Mteule Mch. Penman amepata ushindi dhidi ya mshindani wake wa karibu Mch. Karl Richard.