
Askofu wa KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu leo tarehe 26/09/2021, amejumuika na Washarika wa Usharika wa Bumbuli Jimbo la Kusini katika Ibada ya Jumapili, Ibada hiyo ilikuwa na matukio mbalimbali.

Harambee: Imefanyika Harambee katika Usharika wa Bumbuli yenye lengo la kuchangisha pesa zitakazo saidia kukamilisha ujenzi wa Kanisa jipya unaoendelea Usharikani hapo.Usharika wa Bumbuli ni miongoni mwa Sharika za KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ulioko katika jimbo la Kusini lenye Sharika 20. Usharika huu ulitimiza miaka 100 ya Injiri mwaka 1999 na hivi sasa una miaka 122.
Katika harambee hiyo ambayo Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu ndiye aliyekuwa mgeni rasmi kiasi cha Tsh 1,457,500/= kilipatika huku ahadi ikiwa Tsh 7,861,000 na kufanya jumla kuu kuwa Tsh. 9,318,500/=.

Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewashukuru Washarika waliopo ndani na nnje ya usharika wa Bumbuli kwa namna walivyo jitoa kwa hali na mali ili kuwezesha ujenzi huo wa Kanisa . Askofu Dkt Mbilu kipekee amemshukuru Waziri wa Nishati na Mbunge wa Jimbo la Bumbuli Mhe. January Makamba kwa mchango wake alio ahidi.

GHARAMA ZA UJENZI: Gharama za ujenzi zinakadiriwa kuwa Tsh. 1,200,000,000 (Bilioni moja na milioni miambili. Kabla ya harambee iliyo fanyika leo jumla ya Tsh 46,592,205.14 zimechangwa na washarika kutoka ndani na nnje ya Usharika wa Bumbuli.

Katika salamu za Waziri wa Nishati na Mbunge wa Jimbo la Bumbuli Mhe. January Makamba zilizotolewa na Katibu wa Mbunge Jimbo la Bumbuli ndugu Mikidadi Mgeta amesema Mhe January Makamba atawasilisha kiasi cha Tsh 5,000,000 (Milioni tano) .

Ibada ilihudhuriwa na Wachungaji, Wainjilisti, Mashemasi, Kwaya ya Walawi Gospel Group and Outreach kutoka Arusha, Washarika pamoja na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Usharika wa Bumbuli.



