
Leo tarehe 16 Oktoba 2021 kumefanyika mahafali ya 32 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Lwandai inayomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, ambapo wanafunzi 41 (wavulana 23 na wasichana 18 ) wamehitimu. Mgeni rasmi katika mahafali hayo alikuwa ni Mhasham Askofu, Dkt Msafiri Joseph Mbilu aliyewakilishwa na Msaidizi wa Askofu , Mchungaji Michael Mlondakweli Kanju. Mahafali hayo yalifana sana yakipambwa na vishirikisho mbalimbali toka kwa wahitimu na wanafunzi wengine.

Wanafunzi wa Sekondari wanaotarajia kuhitimu elimu ya kidato cha nne mwaka huu wametakiwa kutumia vizuri muda wao, kushikamana na kuwa na mbinu mahususi zitakazo wasaidia kufauru kwa pamoja katika mitihani yao itakayo fanyika baadae mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa leo na Msaidizi wa Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mchungaji Michael Mlondakweli Kanju alipokuwa akizungumza kwenye mahafali hayo.

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Jamii Mchungaji Dkt. William Kopwe akitoa salamu za Ofisi Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki amewapongeza walimu wa Shule ya Sekondari Lwandai kutokana na jitihada zao zinazochangia maendeleo makubwa ya taaluma na nidhamu Shuleni hapo.

Sambamba na hilo amepongeza miradi inayoendeshwa Shuleni hapo ambayo inalenga kuwaandaa wanafunzi katika stadi za maisha zitakazo wasaidia kujiajiri na kujitegemea.
Aidha Mch. Dkt. Kopwe, ametoa wito kwa walimu kuendelea na juhudi za kuitangaza shule katika namna mbalimbali ili kuwaleta wanafunzi Shuleni hapo.

Mzazi rasmi ndugu Rogers Mngazija akiwakilisha wazazi wengine amewasihi wahitimu kutumia maarifa na ujuzi waliopewa na walimu wakati wa kufanya mitihani ili wafaulu vizuri na baada ya mitihani hiyo watakapo rejea nyumbani wakajichunge na kujitunza kwani Jamii inawategemea.

Katika risala iliyo somwa kwa mgeni rasmi wanafunzi hao wanao hitimu wameeleza kuwa moja ya mafanikio ni uwezo wao mkubwa wa kitaaluma kutokana na uwepo wa walimu bora ambao ndio sababu ya Shule hiyo kushika nafasi ya 7 kati ya shule 60 kiwilaya katika mtihani wao wa utamirifu (mock) uliofanyika mwezi wa tano. Wameongeza kuwa wamepata maaarifa ambayo walipaswa kuwa nayo na wanaamini yatawasaidia katika kupambana na changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.

