
Mkuu wa Jimbo la Pwani KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Thadeus Ketto amesema kuwa Halmashauri kuu ya KKKT-DKMs haijakosea kutoa mwaka 2022 kuwa mwaka wa wanawake katika Dayosisi kutokana na mipango na mikakati mizuri waliyoiweka.

Ameyasema hayo kwenye Ibada ya Jumapili katika Usharika wa Kana akimuwakilisha Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kwenye uzinduzi wa mwaka wa wanawake katika Jimbo la Pwani na kuongeza kuwa uongozi wa Jimbo na Dayosisi kwa ujumla utawaunga mkono katika kuhakikisha malengo waliyo jipangia yanakamilika.
Hata hivyo katika kuunga mkono jitihada za kukabiliana na deni la Dayosisi Kitengo cha Wanawake Jimbo la Pwani kimeweka alama ya uzinduzi wa mwaka wanawake kwa kukuunga mkono katika kupunguza deni la Dayosisi kwa kutoa kiasi cha shilingi Milioni moja.

Kwa nyakati tofauti Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Dkt, Msafiri Joseph Mbilu amekuwa akitoa wito kwa Wanawake wote kuupokea mwaka huo kuanzia kwenye ngazi za Mitaa, Sharika, Majimbo hadi Dayosisi kwa kuamini kuwa Wanawake wataweka mipango mbalimbali ili kuuenzi huku kauli mbiu inayoongoza mwaka wao ni kutoka kitabu cha Waamuzi 5:12a “Amka, amka, Debora; amka, amka, imba wimbo”.

Wanawake hao wameushukuru uongozi wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki pamoja na Halmashauri Kuu ya Dayosisi kwa kutangaza mwaka 2022 kuwa mwaka wa Wanawake. Katika utaratibu wa kuthamini na kuhamasisha makundi ya waumini katika Dayosisi, Halmashauri Kuu KKKT-DKMs katika kikao chake cha tarehe 09-10/12/2021 ilipitisha na kuamua kuwa mwaka 2022 uwe mwaka wa Wanawake wa KKKT-DKMs hii ikiashiria kuwa Wanawake ni Jeshi kubwa na lililo imara hivyo wanao uwezo wa kuweka mipango mbalimbali endelevu ili kuinua na kuijenga Dayosisi.

Idara ya Jinsia na Watoto kitengo cha Wanawake KKKT-DKMs kinajishughulisha na mambo ya kiroho, kiuchumi, kielimu na haki kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa. Haya yote yanafanyika katika ngazi ya familia, Kanisa na jamii kwa ujumla. Katika jimbo la Pwani kitengo hicho kinaundwa na Sharika 13, kati ya hizo kuna sharika Teule mbili ambazo ni Usharika wa Bethania na Misioni ya Ng`ambo ya Mto Pangani. Idara inafanya kazi chini ya Kurugenzi ya huduma za jamii.

Shughuli zinazofanywa na Kitengo hiki ni kuwajenga na kuwaimarisha wanawake kiroho, kuwaelimisha wanawake namna ya kujikomboa kiuchumi na kuwa na maendeleo bora katika jamii, kusimamia shughuli za miradi midogomidogo ya wanawake katika Sharika na Mitaa, kuwalea na kuwaongoza Watoto katika njia ya Kikristo, kazi mbalimbali za kidiakonia, kusimamia na kuongoza maombi ya Dunia, Sikukuu ya Mikaeli na Watoto pamoja na maombi ya Adventi kila mwaka.

Kwa upande mwingine mwenyekiti wa wanawake Jimbo la Pwani - Bi. Mercy Mushi amesema kuwa Idara imejiwekea mipango kamila kuwasaidia kufanikisha lengo kuu na malengo mahususi ya mwaka wa wanawake 2022 huku lengo kuu likiwa ni kufanya misioni maalum kuanzia kwenye mitaa, sharikani hadi kwenye Jimbo. Malengo mahusussi ni kuwajengea wanawake uwezo wa kujiamini katika kuhubiri, kufundisha, kuimba ili kutumia vipawa walivyo jaliwa na Mungu.
Kuimarisha uchumi wa wa wanawake kwa kufanya semina za ujasiriamali na VICOBA. Kuimarisha uchumi wa kitengo cha wanawake kwa kusimamia miradi mbalimbali kama mradi wa mashine ya kukoboa na kusaga na kusaidiana kwa kupeana mitaji na baadaye kuirejesha,
Pia jimbo la Pwani lina miradi ifuatayo: madarasa ya ushonaji, kutengeneza batiki, mapishi ya vitafunwa, mradi wa kukodisha viti na kukodisha fremu ya duka.Kuwapa wanawake stadi (ujuzi) wa uongozi kwa kufanya semina za uongozi na wanawake kufanya huduma za kiroho kwa kufanya diakonia kwa kuwatembelea wanyonge/wagonjwa na kufarijiana katika matukio ya kijamii kama misiba na majanga.
Bi. Mercy Mushi ameongeza kuwa katika kutekeleza malengo mahususi idara hiyo imejiwekea mikakati ifuatayo: Kuandaa semina za wanawake za kuwajengea kujiamini, ujasiri na kutumia vipawa walivyonavyo.Kufanya safari za kujifunza ndani na nje ya Dayosisi. Kuandaa kongamano ambalo litakuwa la kujifunza neno la Mungu, michezo na maonesho ya kazi za wanawake. Kuanzisha vikundi vya VICOBA kwa Sharika ambazo hawana vikundi hivyo. Kuanzisha miradi mipya ya kitengo cha wanawake. Kufanya semina za uongozi na kuwapa ujuzi wanawake vijana (mentorship). Kushiriki katika kufanya Uinjilisti wa nyumba kwa nyumba, mikutano ya kiroho Sharikani hadi Jimboni na kutoa huduma za kiroho kwa kushirikiana na kamati za Misioni na Uinjilisti.
Katika mwaka huu Idara itaweka alama kuanzia ngazi za mitaa, Sharika, Jimbo hadi Dayosisi. kama ifuatavyo; Usharika wa Kana – Kununua Kinanda cha Usharika. Usharika wa Makorora – kuongeza viti 120 usharikani na Darasa la ushonaji. Usharika wa Pangani – Kujenga jiko la usharika. Usharika wa Maramba – Kushona majoho 38 ya wazee wa Kanisa. Usharika wa Kisosora – Kujenga darasa la ushonaji. Usharika wa Mikanjuni – Kununua maturubai manne (4) na viti. Usharika wa Kange – Kujenga madarasa mawili ya Shule ya Jumapili (Sunday School). Usharika wa Duga – Kuweka madirisha na tiles nyumba ya mtumishi. Usharika wa Pongwe – Kukamilisha (Finishing) jengo la darasa la Shule ya Jumapili. Usharika wa Amboni – Kushona joho la mtumishi. Usharika wa Duga maforoni – kushona vitambaa vya madhabahuni. Usharika wa Bethania – Gari la Usharika.
Kwa alama ya pamoja katika jimbo kutanunuliwa kiwanja kikubwa ambacho kitajenga nyumba (apartments) na ukumbi. Bajeti ya mwaka kwa Jimbo na Sharika zake ni shilingi milioni sabini (70). Jimbo la Pwani linakadiriwa kuwa na wanawake 5,765, ambapo kila mwanamke anatakiwa kutoa kiasi cha shilingi elfu kumi (ambapo sh. 5,000 ngazi ya Dayosisi, na sh. 5,000 ngazi ya Jimbo) pia watatoa michango mingine kulingana na mipango waliyojipangia katika Sharika zao.

Naye mratibu wa Idara ya Jinsia na Watoto KKKT-DKMs- Mch Happyness Diu ambaye ndiye aliyehubiri katika Ibada hiyo amewataka wanawake kusimama katika nafasi zao kama waombaji, kwani kwa kufanya hivyo Kanisa, Dayosisi, ndoa pamoja na familia kwa ujumla zitasimama imara na kuwa na amani. Akikazia katika suala la maombi alisema kuwa suala la maombi ni la kila mtu na tena ni endelevu hatupaswi kuchoka wala kukoma kuomba maana Mungu kwa wakati wake anajibu maombi yetu. Hivyo tuombe katika jina la Yesu nasi tutapewa maana ni jina lipitalo majina yote.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa kitengo cha wanawake KKKT-DKMs Bi. Christina Peter ameushukuru uongozi wa Dayosisi, Jimbo na Sharika kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata pale wanapofika kwa msaada na ushauri huku akiwashukuru Wachungaji, Mashemasi, Parish workers, Wainjilisti, mabaraza ya wazee wa Kanisa na washarika mmoja mmoja kwa ushirikiano wao kuhakikisha kazi za Idara hiyo zinaendelea.
Hata hivyo kipekee amewashukuru wanawake wote kwa namna wanavyo jitoa hata katika changamoto mbalimbali zinazowakabili hawakukata tamaa wameendelea kumtumikia Mungu kwa uaminifu mkubwa kwakuwa wanawake wamtegemeao Bwana ni jeshi kubwa Zab. 68:11.

