leo tarehe 12/06/2022 Msaidizi wa Askofu KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Michael Mlondakweli Kanju  ameongoza  Ibada ya Jumapili na harambee ya ujenzi wa Kanisa la Mtaa wa Sakura ambao ni senta ya Usharika Mteule wa Ng'ambo ya Mto Pangani.

 Katika Mahubiri yake  alisoma Neno la Mungu kutoka kitabu cha Nabii Isaya 41:14-18. huku akiwatia moyo   Washarika wa Mtaa huo na kuwasihi wasijione wanyonge kwani ahadi ya Mungu anayoitoa kwa wana wa Israeli juu ya kuwainua na kuwatoa katika utumwa na kuwafanya taifa kubwa japokuwa wanaonekana kama wadudu ndio ahadi wanayopewa Washarika hao kuwa Mungu atawainua na hawataonekana wadogo tena. Tena hata katika hatua za ujenzi wa Kanisa hilo Mungu atawashindia na watafanikiwa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

 

 Hata hivyo  Washarika wa Usharika Mteule wa Ng'ambo ya Mto Pangani Mtaa wa Sakura  walianza harambee hiyo kwa   kumkaabidhi Msaidizi wa Askofu Mch. Michael Kanju ambaye ndiye aliyekuwa  Mgeni rasmi jumla ya Tsh. 10,000,000/=.Baada ya harambee yote kufanyika kiasi cha Tshs. 20,753,550/= kilipatikana  Ikiwa fedha taslimu ni Tshs. 12,616,550/ huku ahadi ikiwa  Tshs. 8,137,000/=

Katika Ibada hiyo Msaidizi wa Askofu Mchungaji Michael Kanju aliambatana na Mkuu wa Jimbo la Pwani Mch. Thadeus A. Ketto ambaye ndiye aliyeongoza Liturgia.