Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Kati Dkt. Solomon Jacobo Massangwa amemshukuru na kumpongeza Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, kwa kukubali kuwapokea washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania waliohama kutoka KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa Enndulen-Ngorongoro na kuhamia KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki katika Jimbo la Tambarare Usharika wa Handeni Mtaa wa Msomera.

Askofu  Dkt.  Massangwa ametoa shukrani hizo hapo jana tarehe 13/12/2022 katika Ibada maalumu iliyofanyika katika Jimbo la Tambarare Usharika wa Handeni Mtaa wa Msomera ya kuwakabidhi na kuwapokea washarika hao waliohama kwa hiari yao kutoka Ngorongoro ili kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo.

Kwa upande wake Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Mbilu ameipongeza Serikali kwa namna ilivyoboresha miundo mbinu na huduma mbalimbali zinazopelekea watu wa Msomera kufurahia maisha katika eneo hilo.

 Askofu Dkt. Solomon Massangwa pamoja na Askofu Dkt. Msafiri Mbilu  wakiwa kwenye Chumba cha Computer katika Shule ya Sekondari Msomera 

 

“Sisi kama Kanisa tumeona tufike hapa kuwapokea rasmi washarika wa KKKT ambao walikuwa wanaabudu  katika Dayosisi ya Kaskazini Kati kule Ngorongoro-Arusha na hivyo wamefika mahali hapa Msomera na sisi tumekuja kuwapokea rasmi na katika kuwapokea huku tunamshukuru Baba Askofu Dkt. Solomon  Massangwa aliyekuwa  kiongozi wa washarika hawa katika eneo lile la Ngorongoro amefika siku hii ya leo kutukabidhi rasmi washarika hawa ” Alisema Askofu Dkt. Mbilu.

Hata hivyo Askofu Dkt. Mbilu ametoa ahadi ya kupeleka ombi maalumu kwa Halmashauri Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki itakayoketi hivi karibuni ili Mtaa huo wa Msomera upewe hadhi ya kuwa Usharika Mteule wa Msomera.