Leo tarehe 10/10/2021 Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Dkt Msafiri Joseph Mbilu ameongoza Ibada  ya sikukuu ya mavuno, katika  Jimbo la Pwani, Usharika wa Kana.

Akihubiri neno la Mungu kwenye Ibada hiyo kutoka kitabu cha Mwanzo 4:2b-7 Askofu Dkt. Mbilu aliwakumbusha waumini wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kuwa na desturi ya kuandaa sadaka wanazozipeleka madhabahuni  kwa Bwana ili Mungu aweze kuzitakabali na kuruhusu baraka zake kwenye maisha yao.

Awali akitoa salamu za Ofisi Kuu ya Dayosisi kwa washarika wa Kana, Askofu Dkt. Mbilu aliwakumbusha wana KKKT-DKMs umuhimu wa kumtumikia Mungu kupitia matoleo hasa akikazia mfuko wa maendeleo ambao unaviwezesha vituo mbalimbali vya Dayosisi kuihudumia jamii.

 

Aidha aliwasilisha salamu kutoka kwenye mkutano ulioandaliwa na Lutheran Mission Cooperation (LMC) ambako alihudhuria ukiwa na lengo la kukumbusha juu ya mafundisho potofu yanayo shamili katika kipindi hiki, Askofu Dkt. Mbilu aliendelea kuwakumbusha wakristo na waumini wa KKKT kujiepusha na mafundisho ya namna hiyo ambayo yanashika kasi katika nyakati tulizo nazo.