
ELCT-NED FAMILY BONANZA, lililoratibiwa na Kurugenzi ya Uchumi, Mipango na Maendeleo Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), limefanyika tarehe 13 Desemba 2025 katika Hoteli ya Mbuyukenda, jijini Tanga, likiwakutanisha waumini, wadau mbalimbali pamoja na familia zao kutoka maeneo mbalimbali.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Uchumi, Mipango na Maendeleo wa KKKT-DKMs, Bi. Pendo Lauwo, aliwashukuru kwa dhati washiriki wote waliojitokeza kushiriki Bonanza hilo pamoja na wadau waliotoa michango yao, akisisitiza kuwa mshikamano na moyo wa kujitolea uliooneshwa ni kielelezo cha umoja wa kitaifa katika kulijenga kanisa na jamii kwa ujumla. Alibainisha kuwa mafanikio ya Bonanza hilo yametokana na ushirikiano wa pamoja kati ya kanisa, wadau na jamii.
Bonanza hilo lililenga kuimarisha umoja, ushirikiano na mshikamano wa kifamilia, sambamba na kukusanya fedha zitakazotumika kufanikisha KKKT-DKMs Marathon inayotarajiwa kufanyika mwaka 2026. Aidha, sehemu ya mapato yaliyopatikana yameelekezwa kusaidia watoto wenye mahitaji maalum, hususan watoto wenye changamoto ya usonji (Autism), kupitia ununuzi wa vifaa vya Physiotherapy (tiba ya viungo) kwa ajili ya Kituo cha Irente Rainbow School.
Kupitia tukio hili, Kanisa limeonesha kwa vitendo dhamira yake ya kushiriki katika maendeleo ya kijamii, likisisitiza umuhimu wa upendo, huruma na mshikamano wa kitaifa katika kuwajali watoto wenye mahitaji maalum, ambao ni sehemu muhimu ya jamii na rasilimali ya Taifa.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi wa tukio hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanga, Bi. Angela Henry Mono, ametoa wito kwa jamii kuendelea kuwajali na kuwaunga mkono watoto wenye mahitaji maalum, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha watoto hao wanapata haki, ulinzi na fursa sawa za maendeleo.
Bi. Mono alieleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini, hususan KKKT-DKMs, katika kufikia na kuboresha ustawi wa watoto wenye mahitaji maalum nchini. Aidha, aliipongeza Dayosisi kwa kazi kubwa na ya mfano inayofanya ya kuwahudumia makundi yenye uhitaji, akibainisha kuwa mchango wa kanisa unaunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha ustawi wa jamii na maendeleo jumuishi ya Taifa.


