Dayosisi yetu imepata heshima kubwa ya kushiriki katika Mkutano wa Kanda ya Afrika ulioandaliwa na United Evangelical Mission (UEM), uliofanyika katika mji wa Gaborone, nchini Botswana kuanzia tarehe 23 Februari hadi 1 Machi mwaka huu.

Katika mkutano huu muhimu dayosisi yetu  imewakilishwa na viongozi na wajumbe wafuatao:

  1. Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu

  2. Mch. Happiness Diu – Mjumbe wa Bodi ya UEM Afrika anayewakilisha wanawake

  3. Elvina Riziki – Mwakilishi kundi la  vijana

Mkutano huu uliwakutanisha washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa lengo la kujadili masuala ya huduma, umoja, uinjilisti, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa makanisa yaliyo chini ya UEM. Ilikuwa ni nafasi ya kubadilishana uzoefu, kujifunza, na kupanga mikakati ya kuendeleza kazi ya Mungu.

Katika mkutano huo, Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu alipata fursa ya kuwa mnenaji wa Neno Kuu la UEM. Ujumbe wake ulijikita katika andiko kutoka Injili ya Mathayo 7:5 lisemalo: “Itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”

Kupitia Neno hili, Baba Askofu alisisitiza umuhimu wa kujitathmini, toba, na unyenyekevu katika huduma na maisha ya kila siku. Aliwahimiza washiriki kuanza mabadiliko ndani yao kabla ya kuwakosoa au kuwaongoza wengine, akisisitiza kuwa uongozi wa kweli huanzia katika usafi wa moyo na nia njema.

Tunamshukuru Mungu kwa safari hii, uwakilishi mzuri wa Dayosisi yetu, na kwa mafanikio ya mkutano huu. Tunaamini kuwa matunda ya mkutano huu yataonekana katika kuimarika kwa huduma zetu na katika kukuza umoja wa Kanisa la Mungu barani Afrika na Duniani kote.