Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, leo tarehe 04 Machi 2026, amezindua rasmi Bodi ya Mfuko wa Pension iliyochaguliwa na Halmashauri Kuu ya Dayosisi.
Baada ya uzinduzi huo, Bodi ilifanya kikao chake cha kwanza katika Kituo cha Mbuyukenda, mkoani Tanga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Baba Askofu alieleza kuwa mfuko huo umeanzishwa kwa ajili ya kuhakikisha mustakabali bora wa watumishi wa kiroho wanaolitumikia Kanisa. Alisisitiza kuwa mfuko huo unahitaji usimamizi imara, maono makubwa, na uwajibikaji wa hali ya juu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Alifafanua kuwa jukumu kuu la Bodi hiyo ni kuhakikisha watumishi wa kiroho walioitumikia Dayosisi wanatunzwa na kupongezwa ipasavyo pindi wanapostaafu utumishi wao. Aidha, aliitaka Bodi kutoa elimu kwa Wakristo wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kuhusu umuhimu wa Mfuko wa Pension na kuhamasisha ushiriki wao kikamilifu.
Baba Askofu aliongeza kuwa masuala ya watumishi yanapowekwa mikononi mwa waumini, kupitia vipawa vyao na moyo wao wa kujitoa, yanaweza kuleta mafanikio makubwa katika kuwahudumia na kuwajali watumishi wa Kanisa.
Kwa upande wake Mwenyekiti Bw. Dickson Mosi, mara baada ya kupokea wajibu huo ameahidi kutumia vipawa na utaalamu wao kubuni vyanzo vipya vya mapato, kuboresha vilivyopo, pamoja na kusimamia Mfuko huo kwa uadilifu na uwazi kwa manufaa ya Dayosisi na watumishi wake.


