Uncategorised
- Details

Mnamo tarehe 26/11/2020 Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu alichaguliwa kuwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.
Askofu Dkt. Mbilu alichaguliwa kuwa Askofu wa KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki baada ya kufanyika Mkutano Mkuu wa 3 baada ya miaka 125 ya Injili ulioanza tarehe 25-26/11/2020 mkutano uliokuwa na ajenda kuu moja ya Uchaguzi wa Askofu mpya wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na viongozi wengine.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati maalumu ya kuratibu shughuli za mkutano mkuu wa uchaguzi alikuwa Askofu Mstaafu Dkt. Paulo Akyoo toka KKKT Dayosisi ya Meru ambaye baada ya uchaguzi alimtangaza Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu aliye chaguliwa na Wajumbe wa mkutano Mkuu kuwa Askofu mteule wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa kupata kura 194 sawa na 89.4% .
Askofu Mteule alimteua Mch Michael Mlondakweli Kanju ambaye alithibitishwa na mkutano Mkuu kwa kura ya Siri na kufanikiwa kupata kura 170 Kati ya 210 sawa na 80.9%. Kura hizo ni zaidi ya 2/3 ambalo ni hitaji la kikatiba. Aidha Mkutano Mkuu ulichaguwa wajumbe wa Halmashauri kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki baada ya kupatikana kwa Halmashauri kuu hiyo ilitimiza wajibu wake wa Kikatiba wa kuchaguwa Wakuu wa Majimbo na kuwaleta mbele ya Mkutano mkuu.
Ikiwa tayari umetimia mwaka mmoja leo tarehe 26/11/2021 Askofu Dkt Msafiri Joseph Mbilu anawashukuru wana KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa ushirikiano mzuri waliouonesha kwa kuunga mkono kazi mbalimbali zinatotekelezwa katika Dayosisi.
Shukrani hizo amezitoa alipokuwa anafanya mahojiano maalumu na kituo cha redio cha Utume Fm pamoja na kitengo cha Habari na mawasiliano cha KKKT-DKMs.
Askofu Dkt. Mbilu ambaye alizaliwa tarehe 9 Mei, 1968 katika kijiji cha Kwang’wenda, Soni, Wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga, alianza kukalia kiti hicho cha uaskofu tarehe 09/05/2021, siku ambayo aliingizwa kazini.
Askofu Dkt. Mbilu alibarikiwa kuwa Mchungaji Februari 19, 1995, alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Msingi Kwang’wenda, Lushoto. Mwaka 1985-1988 alipata elimu ya sekondari katika shule ya sekondari Namfua iliyopo wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro. Alipata elimu ya Theologia, Chuo cha Theologia, Makumira mwaka 1990- 1994 na kumaliza masomo ya General Certificate in Theology.
Mwaka 1997 alijiunga na masomo ya shahada ya Theolojia chuo kikuu cha Makumira na kuhitimu mwaka 2000. Alipata shahada ya uzamili ya Theolojia mwaka 2000-2002 huko Norway, katika chuo cha Stavanger School of Mission and Theology.
Mwaka 2006-2012 alijiunga na chuo kikuu cha Kirchliche Hochschule Wuppertal cha nchini Ujerumani ambapo alitunukiwa shahada ya uzamivu katika Theolojia. Kabla ya kufikia nafasi hiyo amewahi kuwa Mwalimu Chuo cha Biblia Vuga 1994-1997 na pia amewahi kuwa Mchungaji Kiongozi Usharika wa Mombo, mwaka 1997-1999 na Usharika wa Korogwe 2003.
Aliwahi pia kuwa Mkuu wa Jimbo la Kaskazini na Mchungaji wa Usharika wa Mlalo kuanzia mwaka 2004 hadi 2006, na mwaka 2012 alikuwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kange. Askofu Dkt. Mbilu amewahi kuwa Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira 2012- 2015.
Pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa kituo cha Tanga cha Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastiani Kolowa, (SEKOMU) mwaka 2015-2016. Vilevile alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho kati ya mwaka 2016 hadi 2018 na mhadhiri chuoni hapo katika masomo ya Agano Jipya na Lugha za Biblia (Kigiriki).
Hadi siku anachaguliwa kuwa Askofu Mteule, Askofu Dkt. Mbilu alikuwa Mhadhiri Mwandamizi katika chuo kikuu cha Silliman, akifundisha masomo ya Agano Jipya na Lugha za Biblia (Greek na Hebrew).
NDOA
Alifunga ndoa na Mary Joseph Jali Desemba 9, 1995 na wamejaliwa kupata watoto watatu, Sarah Mbilu, Joseph Mbilu na Jackskon Mbilu.
WAKUU WA MAJIMBO
Pia Halmashauri Kuu ya Dayosisi, iliwachagua Mch. Frank Mntangi kuwa Mkuu wa Jimbo la Tambarare, Mch. Issai Amasia Mweta kuwa Mkuu wa Jimbo la Kusini, Mch. Anderson Kipande kuwa Mkuu wa Jimbo la Kaskazini na Mch. Thadeus A. Ketto Mkuu wa Jimbo la Pwani. Wakuu hawa wa majimbo walitangazwa wazi na kupokelewa rasmi katika Mkutano Mkuu wa Dayosisi uliofanyika Kanisa Kuu Lushoto (Cathedral) tarehe 25-27/11/2020.
- Details

Mwanamke mwema ni taji la mumewe ;bali aaibishae ni kama kuoza mifupani mwake. Mithali 12: 4 haya yamehubiriwa leo tarehe 26/11/2021 na Mchungaji Sabina Lumwe katika ibada ya ufunguzi wa warsha ya wake wa wachungaji na mashemasi kutoka Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Dayosisi ya Mashariki na Pwani. ambapo Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ndiye aliyekua mgeni rasmi wa warsha hiyo inayofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa SEKOMU-Lushoto Tanga
Askofu Dkt Msafiri Mbilu wakati wa ufunguzi amesoma neno kutoka kitabu cha Mithali 12:2 na kusisitiza wake wa Wachungaji waendelee kuwa taji kwa kufanya mema na kumcha Mungu sambamba na hilo amewasisitizia kutokujichanganya kwengine bali kukumbuka wao kuwa ni Walutheli.

Hata hivyo baba Askofu amesisitiza utanashati, upole, uaminifu na kutopenda utajiri wa haraka haraka ni vitu muhimu kwa mke wa Mchungaji, mbali na hayo mke wa Mchungaji anapaswa kuwa mchakarikaji na kuwa mpambanaji kwenye suala zima la kuimarisha kipato cha familia.

Warsha hii imeandaliwa na UEM kwa kushirikiana na Dayosisi ya Kaskazini Mashariki pamoja na Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
UEM: United Evangelical Mission ni chama Cha kiinjili Cha kimisioni kilichoanzishwa miaka 25 iliyopita na wamisionari kutoka Ujerumani wa Rhenish na Betheli ambao walifika Africa, na Asia kwa ajili ya kuanzisha shughuli za Dini. Katika Africa walifika katika nchi 7 ambazo ni Tanzania, DR Congo, Africa ya Kusini, Botswana, Cameroon, Namibia na Rwanda kukiwa na madhehebu 15. Katika Tanzania inawakilishwa na Makanisa 4 ya KKKT ambayo ni KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani pamoja na KKKT Dayosisi ya Karagwe.

Aidha Chama hiki kinashughulika katika nguzo tano ambazo ni Uhusiano/ Undugu, Diakonia, Uinjilishaji, Utetezi pamoja na Maendeleo.
- Details

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kama msimamizi wa mali za Dayosisi kupitia halmashauri Kuu ambayo yeye ni mwenyekiti wake amesema kuwa watahakikisha majibu ya zilipo fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya Dayosisi ambazo hazikutumika kama ilivyokusudiwa yanapatikana.

Katika kufanikisha hilo amesema kuwa watumishi mbalimbali ikiwemo wachungaji waliokuwa wakiwajibika kusimamia fedha hizo wataulizwa hata ikibidi kwa ukali.
Page 97 of 124


