Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewataka wachungaji kusimama imara ili kupinga na kukemea mafundisho potofu ya neno la Mungu yanayoletwa na watumishi wa uongo maeneo mbalimbali nchini.

Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo leo tarehe 07/08/2022 akiwa katika Jimbo la Pwani Usharika wa Kana kwenye Ibada ya kubarikiwa na kuingizwa kazini kwenye huduma ya Kichungaji, Mch. Jonathan Denis Hizza na kusema kuwa katika nyakati tulizonazo kumejaa mafundisho ya uongo kutokana na watu mbalimbali ambao wameibuka na kujiita watumishi wa Mungu.

Amesema kuwa watumishi hao hawajaandaliwa katika utaratibu wa kumtumikia Mungu bali wamejiandaa wenyewe jambo ambalo linasababishwa na ukosefu wa ajira hivyo kupelekea mtu anaamua kuvamia Biblia kwa madai ya kufunuliwa na kuanza kufundisha na  kupotosha jamii.

Aidha amemtaka Mchungaji Jonathani Hiza kutambua kuwa ameitwa katika wakati mgumu ambao Kanisa limekumbwa na mafundisho hayo hivyo anapaswa kupinga mafundisho hayo na kuongeza kuwa mchungaji yeyoto ambaye hatokemea mafundisho hayo potofu hafai kwa kazi ya Mungu.

Sambamba na hayo amemkumbusha Mch. Jonathan Hiza kutambua ameitwa kuwatumikia watu wote bila kuwa na makundi katika Kanisa la Mungu huku akimtaka kujishughulisha na miradi mbalimbali ya kiuchumi.

Sehemu ya Washarka wa Usharika wa Kana