Wajumbe 217 kati ya 246 wa Mkutano Mkuu wa tano (5) baada ya Jubilee ya miaka 125 ya Injili KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs) sawa asilimia 88.5% wamemuidhinisha Mchungaji Frank Richard Mntangi kuwa Msaidizi wa Askofu (Dean Mteule) wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Mch. Frank Mntangi ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Jimbo la Pwani, ameteuliwa kuhudumu nafasi hiyo ya msaidizi wa Askofu ambayo kwa sasa inaongozwa na Mch. Michael Mlondakweli Kanju anayestaafu kwa mujibu wa sheria za utumishi za KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.



Akizungumza mara baada ya kuidhinishwa na Mkutano Mkuu, Mch. Mntangi amemshukuru Mkuu wa KKKT-DKMs Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, kwa kumuamini kwenye majukumu mbalimbali ya ukuu wa Jimbo la Tambarare na baadae jimbo la Pwani ambapo pia ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wanadayosisi wote.

Kwa upande wake Msaidizi wa Askofu anayemaliza muda wake Mch. Michael Kanju, amesema ataendelea kushirikiana na viongozi wa Dayosisi ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Dean Mteule, na kuahidi kuendeleza msimamo wake wa kusema kweli na kupinga kauli za wapotoshaji juu ya Dayosisi hii.

Nae Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amemshukuru Dean anayemaliza muda wake Mch. Michael Kanju kwa ushirikiano mzuri alioutoa katika kipindi cha uongozi wake, huku akimpongeza Mch. Frank Mntangi kwa kuidhinishwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu.

Mkutano Mkuu wa tano (5) baada ya miaka 125 ya Injili unafanyika kwa siku tatu Aprili 3-5/04/2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Benjamin Mkapa uliopo katika Chuo cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) kilichopo Magamba wilayani Lushoto.

Kwa mujibu wa Katiba ya KKKT-DKMs ya mwaka 1966 na marekebisho yake ya mwaka 2000 Kanuni ya V kifungu C, Mkutano Mkuu ndio chombo chenye mamlaka ya juu katika Dayosisi yetu.