Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki(KKKT-DKMs), Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ameongoza Ibada ya kumbariki na kumuingiza kazini Mtheolojia Steven Emanuel Mhangwa kuwa Mchungaji, leo 22/11/2025, katika Jimbo la Pwani, Usharika wa Kange.

Awali, Mch. Steven Mhangwa alipaswa kuwa miongoni mwa watheolojia 14 waliobarikiwa kuwa Wachungaji katika Ibada ya Jumapili ya Siku ya Bwana ya 2 Kabla ya Majilio, iliyofanyika katika Usharika wa Kanisa Kuu Lushoto tarehe 16/11/2025. Hata hivyo, kutokana na sababu za kiafya, amebarikiwa leo tarehe 22/11/2025.

Askofu Dkt. Mbilu alieleza kuwa kupitia vikao vya Halmashauri Kuu ya Dayosisi, iliamuliwa kuwa Mashemasi wapatiwe kozi maalum ya Theolojia. Jumla ya Mashemasi 14 walifuzu kwa kiwango kizuri katika kozi hiyo.

Katika mahubiri yake, Askofu Dkt. Mbilu alikazia kuwa huduma ya uchungaji ni kazi ngumu na inahitaji mtu anayesimama katika kweli, akiwa chombo safi cha Mungu katika kulihubiri neno lake. Aliwakumbusha watumishi wa Mungu kuwa kama nabii Isaya, walipaswa kuandaliwa na Roho Mtakatifu ili aweze kulitangaza neno la Mungu ipasavyo.

Ameongeza kuwa uchungaji ni wito, si ajira, na hivyo ni lazima kuufuata kwa moyo wa kujikana na kujitoa. Aliwahimiza watumishi wa Mungu kutokata tamaa wanapokumbana na kubezwa, kutukanwa au changamoto nyingine, kwani wito huu unahitaji uvumilivu na uaminifu hata katika nyakati ngumu hivyo mtumishi anapaswa kusimama imara akihubiri kweli ya Mungu na habari njema kwa watu wake.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa maadili ya uchungaji, akisema kuwa ni jukumu la kila Mchungaji kuyafuata, kuyatii na kusimama imara kuyasimamia.

 Katika Ibada hii, Askofu Dkt. Mbilu aliambatana na Msaidizi wake Mch. Frank Mntangi, Mkuu wa Jimbo la Pwani Mch. Isai Mweta, Mkuu wa Jimbo la Tambarare Mch. John Ndimbo, pamoja na Wachungaji kutoka sharika mbalimbali za KKKT–Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

 Tufuatilie kwenye mitandao yetu ya kijamii:

Instagram: elctned

Facebook Account: North Eastern Diocese

Facebook Page: ELCT–North Eastern Diocese

YouTube: KKKT DKMS Online TV

Website: www.elctned.org

Kwa Maoni na Ushauri:

Simu: +255 743 399 798