Wapendwa  wana KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki yahusu ziara rasmi ya kikazi ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Baba Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo katika Dayosisi yetu kuanzia tarehe 27/07/2022 hadi tarehe 02/08/2022.

 Dhumuni la ziara ya Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo ni kuitembelea KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, kufungua na kuweka mawe ya msingi. Vilevile Baba Askofu Dkt. Shoo atapata wasaa wa kuongea na wana Dayosisi katika maeneo mbalimbali.

 Baba Askofu atawasili katika Dayosisi yetu tarehe 27/07/2022 siku ya jumatano saa 4:00 asubuhi, punde atakapokanyaga ardhi ya Mkoa wa Tanga katika eneo la Bwiko atapokelewa na mwenyeji wake Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu na wana Dayosisi. Ataanza ziara yake siku hiyohiyo ya tarehe 27/07/2022 katika Jimbo la Tambarare kwa kuweka jiwe la msingi la Kanisa jipya katika Usharika wa Mombo muda saa 6:00 mchana.

 Aidha mara baada ya uwekwaji wa jiwe la msingi msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea katika Jimbo la Kusini ambapo Baba Askofu Dkt. Shoo ataongea na wana Dayosisi katika Usharika wa Soni yalipo Makao Makuu ya Jimbo hilo majira ya saa 10:00 jioni. Mara baada ya kuongea na wanadayosisi katika Usharika wa Soni siku hiyohiyo msafara utaelekea Kanisa Kuu Lushoto ambapo Mkuu wa KKKT atapokelewa rasmi kwa Ibada maalum saa 11:45 jioni.

 Tarehe 28/07/2022 msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea Bumbuli kuanzia saa 2:00 – 6:00 mchana, ambapo Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo ataendelea na ziara yake katika Jimbo la Kusini kwa kutembelea Usharika wa Bumbuli, Hospitali ya Bumbuli na Chuo cha Utabibu Bumbuli (BUCOHAs).

Majira ya saa 7:30 mchana hadi saa 12:00 jioni msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea Lutindi ambapo Baba Askofu atapata wasaa wa kuwasalimu washarika wa Lutindi na kutembelea Hospitali ya wagonjwa wa akili Lutindi (Lutindi Mental Hospital).

 Siku ya tarehe 29/07/2022 msafara wa Mkuu wa KKKT muda wa saa 3:00 hadi 6:00 mchana  utaelekea katika Jimbo la Tambarare ambapo itafanyika Ibada katika Usharika wa Korogwe na majira ya saa 7:00 mchana msafara utaelekea Jimbo la Pwani.

 Tarehe 30/07/2022 saa 3:00 – 6:00 mchana Baba Askofu ataweka jiwe la Msingi wa Kanisa la Makorora na kuongoza Ibada ya kipaimara katika Usharika huo wa Makorora.

 Tarehe 31/07/2022 Mkuu wa Kanisa ataongoza Ibada ya jumapili Kanisa Kuu Lushoto kuanzia saa 2:00 – 5:00 asubuhi na majira ya saa 8:00 – 10:00 jioni atatembelea vituo vya Irente Rainbow School, Irente Children’s Home, Irente School for the Blind na Irente Farm.

 Tarehe 01/08/2022 saa 4:00 – 5:00 asubuhi msafara wa Mkuu wa Kanisa utaelekea katika Jimbo la Kaskazini ambapo pia kutafanyika Ibada katika Usharika wa Mlalo na majira ya saa 6:30 -8:00 mchana ataelekea katika Shule ya Sekondari Lwandai ambapo Baba Askofu Dkt. Shoo atafungua tena Jengo la Maabara ambalo lilifanyiwa ukarabati  na majira ya saa 9:00 – 11:00 jioni msafara wa Mkuu wa Kanisa utaelekea katika Chuo  kitarajiwa cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI).

 Wito kutoka kwa Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kwa wana KKKT – DKMs, ni kujitokeza kwa wingi kumpokea Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo sehemu zote atakazopita kuanzia Bwiko, Soni, Lushoto, Mlalo, Bumbuli, Lutindi, Tanga, Korogwe na maeneo yote yaliyotajwa atakapokuwa anatembelea, anafungua, anaweka mawe ya msingi na atakapokuwa anaongea nasi.

 Mwisho kama ilivyo kawaida na desturi ya wana KKKT-DKMs wakati tunapotembelewa na wageni hasa ugeni mkubwa wa Mkuu wetu wa KKKT, Baba Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo, natoa wito tena kwenu kujitokeza kwa wingi tumpokee Mkuu wetu wa Kanisa katika Dayosisi yetu.

 

TANGAZO LA NAFASI ZA KAZI.                                                                   25/06/2022

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki imepata kibali cha ajira za Watumishi wa Kada za afya 18 kwa ajili ya Hospitali na vituo vya afya.

Sifa za waombaji ni kama ifuatavyo;

  1. DAKTARI DARAJA LA II (NAFASI 3)

Waombaji wawe na Shahada ya Udaktari wa binadamu kutoka Vyuo vikuu/ Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali. Waombaji wawe wamemaliza mafunzo ya kazi “internship” ya muda usiopungua mwaka mmoja na kupata usajili kutoka Baraza la Madaktari Tanganyika (Medical Council of Tanganyika)

  1. AFISA MUUGUZI DARAJA LA II (NAFASI 2)

Waombaji wawe na Shahada ya Uuguzi kutoka Chuo Kikuu kinachotambuliwa na Serikali, waliohitimu mafunzo kwa vitendo (Internship) ya mwaka mmoja ambao wamesajiliwa na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (Tanzania Nurses and Midwifery Council).

  1. AFISA MUUGUZI MSAIDIZI DARAJA LA II (NAFASI 2)

Waombaji wawe na Stashahada ya Uuguzi ya muda usiopungua miaka miwili kutoka Chuo kinachotambuliwa na Serikali, waliosajiliwa na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (Tanzania Nurse and Midwifery Council)

  1. TABIBU DARAJA LA II (NAFASI 2)

Waombaji wawe na Stashahada ya Utabibu (Diploma in Clinical Medicine) ya muda wa miaka mitatu kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali.

  1. OCCUPATIONAL THERAPIST II (NAFASI 1).

Kuajiriwa wahitimu wenye Stashahada Mtoa tiba kwa Vitendo kutoka Chuo kinachotambuliwa na Serikali.

  1. MUUGUZI DARAJA LA II (NAFASI 3).

Waombaji wawe na cheti cha Uuguzi cha miaka miwili kutoka katika Chuo kinachotambuliwa na Serikali na Kuandikishwa (Enrolled) na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (Tanzania Nurse and Midwifery Council).

  1. MFAMASIA DARAJA LA II (NAFASI 1)

Waombaji wawe na Shahada ya Famasi kutoka Chuo kinachotambuliwa na Serikali waliohitimu mafunzo kwa vitendo (internship) ya mwaka mmoja na ambao wamesajiliwa na Baraza la Famasi (Pharmacy Council)

  1. MTEKNOLOJIA (DAWA) (NAFASI 1)        

Waombaji wawe na Stashahada katika fani ya Uteknolojia wa Dawa (Diploma in Pharmaceutical Technology) kwa muda wa miaka mitatu kutoka katika chuo kinachotambuliwa na Serikali na ambao wamesajiliwa na Baraza la Famasi (Pharmacy Council)

  1. MTEKNOLOJIA WA DAWA MSAIDIZI (NAFASI 1)

Waombaji wawe na Astashahada katika fani ya Uteknolojia wa Dawa (Certificate in Pharmaceutical Technology) kwa muda wa miaka mitatu kutoka katika chuo kinachotambuliwa na Serikali na ambao wamesajiliwa na Baraza la Famasi (Pharmacy Council)

  1. MTEKNOLOGIA WA MAABARA DARAJA LA II (NAFASI 1)

Waombaji wawe na Stashahada katika fani ya Uteknolojia wa Maabara ya Afya (Diploma in Health Laboratory Science) kwa muda wa miaka mitatu kutoka Chuo kinachotambuliwa na Serikali na ambao wamesajiliwa na Baraza la Wataalamu wa Maabara za Afya (Health Laboratory Practitioners’ Council)

 

 

 

  1. MSAIDIZI WA AFYA (NAFASI 1)

Waombaji wawe wahitimu wa kidato cha nne waliofuzu Mafunzo ya Mwaka mmoja katika fani ya Afya. Afya ngazi ya jamii au mafunzo yoyote yanayofanana na hayo kutoka vyuo vya afya vinavyotambuliwa na Serikali.

MASHARTI YA JUMLA YA WAOMBAJI WA KAZI.

  1. Awe raia wa Tanzania.
  2. Awe na umri usiopunguza miaka 18 na usiozidi miaka 45.
  • Awe na vyeti kamili vya mafunzo ya fani aliyosomea (Cheti cha Kidato Cha Nne, Sita, Taaluma na usajili kamili (Full Registration) au leseni hai ya kufanya kazi ya taaluma husika.
  1. Asiwe mwajiriwa wa serikali au mwajiriwa wa Hospitali za Mashirika ya Dini ambaye mshahara wake unalipwana serikali.
  2. Mwombaji aliyewahi kuajiriwa serikali na kupata cheki namba, atatakiwa kuzingatia utaratibu wa kuomba kibali cha kurejea katika utumishi wa umma na kuendelea kutumia cheki namba baada ya kuach akazi kama ilivyobainishwa kwenye waraka na. CCB.228/271/01 wa tarehe 7 Agosti 2012.
  3. Mwombaji awe na sifa na weledi kwa mujibu wa waraka wa maendeleo ya Utumishi Namba. 1 wa mwaka 2009 kuhusu kada zilizo chini ya Wizara ya Afya kama zilivyoainishwa hapo juu.
  • Waombaji wenye elemavu watapewa kipaumbele katika ajira hii kwa kuzingatia sheria ya watu wenye ulemavu Na. 1 ya mwaka 2010.

MAOMBI YOTE YAAMBATANISHWE NA,

  1. Nakala ya cheti cha kuzaliwa.
  2. Nakala ya cheti cha kidato cha nne au/ na cha sifa au stashahada kulingana na kada ya mwombaji. Kwa aliyesoma nje ya nchi au mitaala ya nje ya nchi waambatanishe cheti cha ithibati kutoka baraza la mitihani Tanzania (NECTA).
  • Nakala ya vyeti vya Taaluma na Transcript, Aidha waliosoma vyuo vya nje ya nchi, waambatishe cheti cha Ithibati kutoka TCU.
  1. Wasifu (CV).
  2. Nakala ya cheti cha Usajili na Leseni hai ya taaluma husika (Full Registration & Valid Licence).
  3. Nakala ya cheti cha Mafunzo kwa vitendo (Internship).
  • Picha ndogo (passport size) moja ya hivi karibuni.
  • Nakala ya kitambulisho cha uraia (NIDA/ Namba ya NIDA).
  1. Iwapo majina yako yanatofautiana katika vyeti vyako Pamoja na cheti cha kuzaliwa na NIDA hakikisha unawasilisha kiapo cha majina (Deed Pool) kutoka kwa Msajili wa viapo na kusajiliwa na Msajili wa hati, wizara ya Ardhi na maendeleo ya makazi.

NAMNA YA KUTUMA MAOMBI.

Maombi yote yatumwe ndani ya wiki mbili tangu tarehe ya kutoka kwa Tangazo hili (mwisho wa kutuma maombi ni Tarehe 03/08/2022).

Maombi yote yatumwe kwa ofisi ya Katibu Mkuu-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki

S.L.P 10 LUSHOTO

Email:This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Leo tarehe 17/07/2022 imekuwa siku ya baraka tele kwa washarika wa Jimbo la Kaskazini ,Usharika wa Mlalo kwani vijana wapatao 116 walipata kipaimara na wanne  4 kati yao walibatizwa.

Katika Ibada hiyo Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ndiye aliye ongoza Ibada hiyo, huku Liturgia ikiongozwa na Msaidizi wa Askofu KKKT-DKMs Mch. Michael Mlondakweli Kanju. 

 Katika Risala ya vijana hao waliobarikiwa iliyosomwa mbele ya Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu vijana hao wametambua jitihada za Baba Askofu pamoja na wasaidizi wake katika kusimamia mambo ya Elimu na Afya.  Hata katika kipindi hiki ambacho Dayosisi inakabiliana na  deni  bado wameona na kushuhudia kazi za maendeleo zikiendelea kufanyika.

Wameeleza kujisikia fahari kuona shule za Dayosisi (Lwandai na Bangala) zikiboreshwa na kuvutia wanafunzi wengi zaidi. Huku wakitambua jitihada za kukifufua kilichokuwa Chuo cha SEKOMU,kwa hatua za awali za kuanzishwa kwa Chuo cha Kati cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) kitakachotoa kozi ya famasia.

KATIKA PICHA: Ibada ya Jumapili kutoka Jimbo la Kusini Usharika wa Ngwelo “B” Bumbuli, ambapo Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ndiye aliyeongoza Ibada hiyo leo tarehe 10/07/2022.

Msaidizi wa Askofu Mch. Michael Mlondakweli Kanju

Mkuu wa Jimbo la Kusini Mch. Issai Mweta