Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewataka Washarika wa Usharika wa Mikanjuni na Wakristo kwa ujumla kuepukana na mafundisho potofu ya neno la Mungu na badala yake kuendelea kumtegemea Mungu katika Maisha yao.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito huo leo tarehe 21/08/2022 katika Ibada ya Jumapili iliyokuwa na tendo la kuwabariki vijana wa kipaimara wapatao 27 iliyofanyika katika Usharika wa Mikanjuni Jimbo la Pwani  ambapo amesema kwa siku za hivi karibuni  Wakristo wamekuwa wakiyumbishwa na kuvutwa na mafundisho ya uongo hivyo kuzitaka Sharika kuandaa Semina za ujasiriamali ili washarika wapate fulsa ya kujifunza namna bora ya kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake Msaidizi wa Askofu KKKT-DKMs Mch. Michael Kanju ambaye ndiye aliye hubiri katika Ibada hiyo amewakumbusha washarika na wakristo kwa ujumla kutumia vyema nafasi zao kwa kutenda haki kwa kila mtu na kuishi maisha ya kumtegemea Mungu zaidi.

Hata hivyo Askofu Dkt. Mbilu ameendelea kuwakumbusha Washarika na watu wote kwa ujumla kujiandaa na zoezi la Sensa ya watu na makazi itakayo fanyika tarehe 23/08/2022 . Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ni pamoja na Kuisaidia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025.

mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa; Taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za Wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali.

 

 

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ameipongeza Bodi inayosimamia Zahanati ya Mtae Mission  pamoja na Washarika wa Usharika huo kwa juhudi walizozifanya na kupelekea zahanati hiyo kufunguliwa tena kwa upya 

ambayo itakwenda kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa eneo.

ASKOFU DKT. MBILU AKIKATA UTEMBE ISHARA YA UZINDUZI WA MNARA WA KENGELE USHARIKA WA  MTAE MTAA WA MAMBO

Pongezi hizo amezitoa leo akiwa katika Jimbo la Kaskazini Usharika wa Mtae kwenye Ibada ya Jumapili iliyokuwa na matukio mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa Mnara wa kengele katika Usharika wa Mtae Mtaa wa Mambo,kufunguliwa kwa Upya Zahanati ya Mtae pamoja na tendo la kuwabariki vijana wa kipaimara ambapo amesema zahanati hiyo ni Muhimu kwa wanamtae na kuipongeza bodi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Aidha Askofu Dkt. Mbilu amesema kufunguliwa kwa upya zahanati hiyo ni kutunza  heshima ya Usharika wa Mtae na Dayosisi kwa ujumla, na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya Afya katika eneo hilo ambapo awali wananchi walilazimika kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Wilaya  Lushoto.

Kadhalika Askofu Dkt. Mbilu amesema azma ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ni pamoja na kutoa huduma za kiroho na za kimwili ikiwemo zahanati hiyo  iliyoanzishwa mwaka 1926 kuwahudumia watu wote tena kwa upendo pindi wanapofika kupatiwa matibabu na hivyo kuitaka bodi ya zahanati hiyo kutokuwa sababu yoyote itakayo pelekea kufungwa tena kwa zahanati hiyo.Katika Ibada hiyo jumla ya vijana wapatao 90 wamebarikiwa na watatu kati yao kubatizwa.

Katika Hatua Nyingine Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito kwa wazazi, walezi na watu wote wanaopenda kujiunga na kozi ya Pharmacy katika ngazi ya Certificate na Diploma kwenye Chuo cha Kolowa Technical Training Institute  chenye usajili namba KOTETI/HAS/249, kutuma maombi kwa kupitia mfumo wa (CAS)  kwenye tovuti ya NACTE  ambapo dirisha la awamu ya pili la Udahili wa pamoja kwa kozi za Afya litafunguliwa hapo kesho tarehe 15 Agosti,2022.

Chuo hiki kipo Wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga na kitatumia majengo ya kilichokuwa Chuo Kikuu cha SEKOMU. 

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewataka wachungaji kusimama imara ili kupinga na kukemea mafundisho potofu ya neno la Mungu yanayoletwa na watumishi wa uongo maeneo mbalimbali nchini.

Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo leo tarehe 07/08/2022 akiwa katika Jimbo la Pwani Usharika wa Kana kwenye Ibada ya kubarikiwa na kuingizwa kazini kwenye huduma ya Kichungaji, Mch. Jonathan Denis Hizza na kusema kuwa katika nyakati tulizonazo kumejaa mafundisho ya uongo kutokana na watu mbalimbali ambao wameibuka na kujiita watumishi wa Mungu.

Amesema kuwa watumishi hao hawajaandaliwa katika utaratibu wa kumtumikia Mungu bali wamejiandaa wenyewe jambo ambalo linasababishwa na ukosefu wa ajira hivyo kupelekea mtu anaamua kuvamia Biblia kwa madai ya kufunuliwa na kuanza kufundisha na  kupotosha jamii.

Aidha amemtaka Mchungaji Jonathani Hiza kutambua kuwa ameitwa katika wakati mgumu ambao Kanisa limekumbwa na mafundisho hayo hivyo anapaswa kupinga mafundisho hayo na kuongeza kuwa mchungaji yeyoto ambaye hatokemea mafundisho hayo potofu hafai kwa kazi ya Mungu.

Sambamba na hayo amemkumbusha Mch. Jonathan Hiza kutambua ameitwa kuwatumikia watu wote bila kuwa na makundi katika Kanisa la Mungu huku akimtaka kujishughulisha na miradi mbalimbali ya kiuchumi.

Sehemu ya Washarka wa Usharika wa Kana

 

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu Dkt. Fedrick Shoo ametoa rai kwa Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kuendeleza jitihada za kukifanya Kiwanda cha uchapishaji cha Vuga Press Publishing House  ambacho kihistoria ni cha kwanza kwa uchapishaji Afrika Mashariki kiendelee na uzalishaji.

Mkuu wa Kanisa ameyasema hayo leo tarehe 02/08/2022 akihitimisha ziara yake katika kiwanda hicho kinacho milikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na kuongeza kuwa kuzingatia historia ya kiwanda hicho na mchango wake katika machapisho jitihada za kupata mashine na mitambo ya kisasa ziendelee kuwepo kwani uwitaji bado ni mkubwa.

Kwa upande wa meneja wa kiwanda hicho Mch. Moses Shemweta amemuelezea mkuu wa KKKT kuwa kiwanda hicho cha uchapaji wa maandiko kilianzishwa mwaka 1912 na wamisionari kutoka Ujerumani katika eneo la Vuga Mission mahali ambapo sasa ni Chuo cha Biblia na Kituo cha Mikutano Vuga. Ameongeza kuwa mwaka 1949 kutokana na changamoto ya miundo mbinu ya barabara na umeme kiwanda hicho  kilihamishiwa katika eneo la  Soni.

Meneja wa kiwanda cha Vuga Press  Mch. Moses Shemweta 

Kiwanda cha Vuga Press kilianzishwa hasa kwa kusudi la kuchapa maandiko mbalimbali ya makanisa, japo baadae kilihusika katika kuchapa maandiko ya Serikali hasa miaka 15 ya kwanza baada ya Nchi ya Tanzania kupata uhuru hadi pale Serikali ilipoanzisha kiwanda chake na kuchukua baadhi ya watumishi kutoka kiwandani hapo.

Pamoja na Uchapaji, kiwanda hicho kilikuwa kiwanda pekee kilichotoa mafunzo ya uchapaji (Printing School) ya uhakika kwa vijana wengi hapa Nchini, hadi pale Serikali ilipoanzisha mafunzo hayo katika chuo cha VETA Dar es salaam pia ikitumia wataalamu kutoka Vuga Press. huku katika kiwanda cha Vuga Press mafunzo hayo yalikoma mwaka 2010.

Aidha kiwanda hicho ndipo ilipokuwa ofisi ya maandiko ya KKKT, kabla haijahamishiwa Arusha. Kwa wakati huu wateja wakubwa wa kiwanda hicho ni Dayosisi yenyewe, makanisa mengine, mashirika na taasisi za serikali na watu binafsi ndani na nje ya mkoa wa Tanga.

Vuga Press inaundwa na idara kuu mbili ambazo ni Utawala na Uzalishaji.   Utawala: Idara hiyo inahusika na uongozi wa kituo, uhasibu, ukadiriaji wa gharama na masoko. Uzalishaji: Idara hii ina sehemu kuu tatu ambazo ni: -UandaajiComposition and Designing. Uchapaji.Ujaladiaji na umaliziaji.

KATIBU MKUU KKKT-DKMs MCH. GODFREY TAHONA WALALAZE

 Vuga Press kama kitega uchumi cha Dayosisi imekuwa ikichangia katika pato na kazi ya Misioni na Uinjilisti ya Dasosisi tangu kilipoanzishwa. Pamoja na kuchangia bajeti ya Dayosisi, kiwanda hicho kilishiriki kikamilifu katika kujenga majengo ya Ibada kwenye maeneo ya misioni ya Masaini, Ununuzi wa kituo cha Martin Luther Garden – Segera pamoja na ujenzi  hoteli ya Tumaini Lushoto.

 Uongozi wa kiwanda hicho umeushukuru uongozi wa KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa jitihada kubwa na mipango mbalimbali kuhakikisha  kituo hicho kinaendelea kuwepo kwa kukijengea uwezo kwa upya, na wanaunga mkono jitihada hizo kwa kutimiza vyema majukumu yao ya kila siku ili kiwanda hicho kiimarike na kuwa na tija kwa Kanisa.

 Awali kabla ya msafara wa Mkuu wa KKKT kufika katika kiwanda hicho Mkuu wa KKKT Dkt. Fredrick Onael Shoo aliagana na uongozi wa KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, wafanyakazi wa Ofisi Kuu katika Ofisi za Makao Mkuu ya Dayosisi.