Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amezindua na kushirikisha Washarika nakala ya taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Dayosisi zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu kubwa na Waumini wa KKKT-DKMs.

Askofu Dkt. Mbilu amezindua nakala hiyo ya taarifa ya hesabu za ukaguzi wa KKKT-DKMs leo tarehe 17/10/2021 katika Ibada ya Jumapili iliyofanyika Kanisa Kuu Lushoto (Cathedral),ambapo pia  alishukuru ushirikiano mkubwa wa UEM katika kukamilisha kazi hiyo.Na kama ishara ya shukrani hizo alikabidhi nakala ya taarifa hiyo kwa Katibu Mkuu wa UEM, Mch. Volker Martin Dally aliyeshiriki Ibada katika Usharika wa Kanisa Kuu Lushoto (Cathedral),ambapo pia alihubiri katika  Ibada zote.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa taarifa kuwa,Taarifa ya ukaguzi wa hesabu imekamilika na taarifa hiyo inaonesha upo upotevu wa mali za Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Hata hivyo taarifa hiyo itapelekwa kwenye Halmashauri Kuu ya Dayosisi mwezi Novemba ili kujadiliwa kwa kina na kuchukuwa hatua stahiki kwa wote waliohusika na upotevu wa fedha na mali za Dayosisi.

Kwa upande mwingine Katibu Mkuu wa UEM Mch Dkt. Volker Martin Dally amemshukuru Askofu Dkt.Mbilu kwa kuweka uwazi juu ya taarifa hiyo na kuahidi kuendeleza urafiki kati ya UEM NA KKKT-DKMs. Ameongeza kuwa amefurahishwa kuona wana KKKT-DKMs sasa wana furaha. 

Katibu Mkuu wa UEM Mch Dkt. Dkt.Volker Dally, amehitimisha ziara yake KKKT-DKMs iliyokuwa na lengo la kurudisha na kuimarisha urafiki na uhusiano kati ya UEM na KKKT-DKMs, ambapo pia kwa nyakati tofauti alipata nafasi ya kutembelea Hospital ya Lutindi pamoja  na Makao Makuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Katibu Mkuu wa UEM Mch Dkt.Volker  Dally katika ziara yake aliambatana na Katibu mtendaji wa UEM Africa   Mch Dkt. John Wesley Kabango pamoja na Naibu Katibu mtendaji wa UEM kanda ya Africa Mch Dkt Ernest William Kadiva.

Naibu Katibu mtendaji wa UEM kanda ya Africa Mch Dkt Ernest William Kadiva.

Katibu mtendaji wa UEM Africa   Mch.Dkt. John Wesley Kabango  

UEM: United Evangelical Mission ni chama Cha kiinjili Cha kimisioni kilichoanzishwa miaka 25 iliyopita na wamisionari kutoka Ujerumani wa Rhenish na Betheli ambao walifika Africa, na Asia kwa ajili ya kuanzisha shughuli za Dini. Katika Africa walifika katika nchi 7 ambazo ni Tanzania, DR Congo, Africa ya Kusini, Botswana, Cameroon, Namibia na Rwanda kukiwa na madhehebu 15. Katika Tanzania inawakilishwa na Makanisa 4 ya KKKT ambayo ni KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani pamoja na KKKT Dayosisi ya Karagwe.