Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Dkt Msafiri Joseph Mbilu amewataka vijana waliopokea kipaimara kusimama imara katika mafundisho sahihi ya neno la Mungu waliyofundishwa kupitia katekisimo ndogo ya Martin Luther, na kamwe wasiyumbishwe na dunia wala mtu yoyote bali wabaki katika Kanisa na zaidi sana waache yale yasiyo mpendeza Mungu,ili mwisho wa maisha haya pamoja na wengine waweze kuwa na sehemu ya kuurithi uzima wa milele.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito huo leo tarehe 18/10/2021 kwenye Ibaba ya Kipaimara ambapo Imekuwa siku ya baraka kwa washarika wa Kabuku Jimbo la Tambarare  kwani vijana wapatao 94 walipata kipaimara  na wanne 4 kati yao walibatizwa.

Liturgia katika Ibada hiyo iliongozwa na Mkuu wa Jimbo la Tambarare Mch. Frank Mtangi, na Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu alihubiri neno la Mungu kutoka kitabu cha Zaburi ya 32:8.

Ibada ilihudhuriwa na Wachungaji, Wainjilisti,Mashemasi,Kwaya,Washarika pamoja na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Usharika wa Kabuku.

Vijana waliopata kipaimara kwenye risala waliyoisoma kwa Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu wamekiri kuwa mafundisho waliyofundishwa kwa kipindi cha miaka miwili yamewajenga kiakili na kiroho na hivyo wapo tayari kupokea majukumu ya kumtumikia Mungu na kuitetea imani yao kama walivyo fundishwa.Huku wakimpongeza Askofu Dkt Mbilu pamoja na msaidizi wake kwa kupokea wajibu wa kuiongoza KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na kuahidi kuwa tayari kuungana na uongozi katika maono ambayo Bwana Yesu Kristo amewapa katika kuiongoza Dayosisi.

Hata hivyo vijana waliopata kipaimara walitoa kiasi cha Tsh 284,000/= kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za KKKT-Dayosisi ya Kaskani Mashariki katika masuala ya elimu.

Salamu kutoka Ofisi Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskani Mashariki katika Ibada hiyo zilitolewa na Msaidizi wa Askofu wa Mch. Michael Mlondakweli Kanju ambapo aliwashukuru washarika kwa namna wanavyo endelea kuiombea Dayosisi yao hata pale inapopita katika kipindi kigumu.