Ikiwa ni mara ya kwanza tangu Kuchaguliwa na Kuingizwa kazini kuiongoza KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewashukuru washarika wa Usharika wa Mkata kwa namna wanavyoendelea kumtumikia Mungu.

Shukrani  hizo amezitoa leo tarehe 23/10/2021, alipokuwa akizindua kisima cha maji katika Usharika wa Mkata, ambapo ameongeza kuwa kuzinduliwa kwa kisima hicho kutapunguza changamoto ya maji katika eneo hilo.

Pamoja na hayo Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu akiwa katika Usharika wa Mkata ameongoza Ibada ya Ufunguzi wa Ofisi ya Usharika ,Ufunguzi wa Kanisa pamoja na Ibada ya Kipaimara.

 

Katika Ibada ya Kipaimara Jumla ya vijana wapatao 20 walipata kipaimara na mmoja kati yao alibatizwa. Ibada hiyo ilihudhuriwa na Wachungaji, Wainjilisti, Mashemasi, Kwaya, Washarika pamoja na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Usharika wa Mkata.

 

Vijana waliopata kipaimara kwenye risala yao kwa Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu wamekiri kuwa mafundisho waliyofundishwa kwa kipindi cha miaka miwili yamewajenga kiakili na kiroho na hivyo wapo tayari kupokea majukumu ya kumtumikia Mungu na kuitetea imani yao na kamwe hawatayumbishwa na mafundisho potofu ya neno la Mungu.