Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu akisaini kitabu cha maombolezo.

Naye atafuta kila chozi katika macho yao,wala mauti haitakuwepo tena,wala kilio,wala maumivu hayatakuwepo tena, kwa kuwa mambo ya kwanza , yamekwisha kupita UFUNUO 21:4.

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Masharika Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu leo tarehe 03/09/2022 ameshiriki Ibada ya mazishi ya Mama Hilda Julius Lugendo ambapo alipata nafasi ya kutoa salamu za pole kwa niaba ya wana KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Marehemu Mama Hilda ni  mke wa Askofu Julius Lugendo wa Kanisa  Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Southern Highlands (Mbeya na Songwe)  huku Ibada ikifanyika katika Kanisa la Kristo Mfalme Madaba (Muheza Tanga).

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Mashariki na Pwani Mch Dkt. Alex Malasusa 
Mama Hilda Lugendo alifariki dunia  alfajiri ya Agosti 17, 2022 Nchini Norway na mwili wake umezikwa leo katika makaburi ya familia yalipo katika kitongoji cha Mbwego Kata ya Mkuzi (Muheza Tanga)


Marehemu Mama Hilda Lugendo katika uhai wake alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Ushirika wa mama wa Kristo (UMAKI) Kanisa  Anglikana Tanzania na amehudumu katika nyadhifa mbalimbali katika Kanisa hilo.

Hata hivyo Kanisa  Anglikana Tanzania limepata na msiba mwingine wa Askofu  wa  Dayosisi ya Mpwapwa, GEORGE YORAM CHITETO ambaye amefariki dunia leo tarehe 03/09/2022 muda mfupi baada ya kutoa mahubiri katika Ibada ya mazishi ya mke wa Askofu Julius Lugendo, Mama Hilda Lugendo.

Askofu George Chiteto  kabla ya mauti kumkuta alihubiri  neno la Mungu  na mahubiri yake yaliwavuta watu na neno lake la mwisho ni mlango umeandaliwa twendeni, Askofu GEORGE YORAM CHITETO mara baada ya kumaliza mahubiri  alipokaa ndipo aliishiwa nguvu na kukimbizwa katika Hospitali ya Teule Muheza na ndipo mauti ilimkuta. Marehemu Askofu  GEORGE  CHITETO aliwekwa Wakfu tarehe 28/08/2022 na amedumu katika Daraja la Uaskofu kwa siku 6.

Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki unatoa  pole kwa Kanisa  Anglikana Tanzania, Baba Askofu Julius Lugendo Familia ya Marehemu, ndugu jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu mzito. Mungu awape nguvu na Faraja ya kweli katika kipindi hiki kigumu.

..............

TAAARIFA YA MSIBA WA  ASKOFU  GEORGE CHITETO WA KANISA ANGLIKANA - MPWAPWA

[Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.-2 Timotheo 4:7-8)]

  1. Kwa masikitiko makubwa, tunawafahamisha kifo cha Mpendwa wetu katika Kristo REV. CAPT. GEORGE YORAM CHITETO, Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Mpwapwa kilichotokea leo tarehe 3 Septemba, 2022 akiwa katika mazishi ya Hilda Lugendo alikuwa ni Mwenyekiti wa Taifa wa Ushirika wa Mama wa Kikristo (UMAKI), Kanisa Anglikana Tanzania, Muheza - Tanga. Baba Askofu CAPT. GEORGE YORAM CHITETO amefikwa na umauti mara baada ya kumaliza kutoa mahubiri kwenye Ibada ya kuuga mwili wa Mama Hilda Lugendo katika Kanisa la Kristo Mfalme Muheza Dayosisi ya Tanga. Alijisikia vibaya na kukimbizwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga ambapo alifariki Dunia.

 

  1. Baba Askofu GEORGE YORAM CHITETO aliwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa, Kanisa Anglikana Tanzania siku ya BWANA ya tarehe 28 Agosti, 2022 katika Kanisa la Watakatifu wote Mpwapwa. Alizaliwa tarehe 7 Desemba, 1962 katika kijiji cha Inzomvu katika Wilaya ya Mpwapwa. Alisoma shule ya msingi Inzomvu kutoka mwaka 1975 hadi mwaka 1981. Baada ya hapo akajiunga na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Chisalu kwa kozi ya Kilimo na ufugaji mwaka 1981. Mwaka 1984 – 1985 alijiunga na Chuo cha Jeshi la Kanisa (Church Army) Nairobi Kenya. Mwaka 1987 aliamuriwa kwa daraja la Ushemasi akatumika katika daraja hilo kwa mwaka mmoja, mwaka 1988 alipata daraja la Ukasisi. Mwaka 1994 alijiunga na Chuo cha Mt. Filipo Kongwa kwa kozi ya Stashahada ya Theologia na kuhitimu mwaka 1996. Mwaka 2005 alijiunga na Chuo kikuu cha Gloucestershire kwa kozi ya Stashahada ya juu. Mwaka 2007-2010 alijiunga na Chuo Kikuu cha Mt. Yohana Dodoma na kuhitimu katika Shahada katika Sanaa ya Theologia na Elimu. Mwaka 2010 – 2011 alihitimu katika Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Theologia kutoka katika Chuo cha Mtakatifu Yohana. Askofu George Yoram Chiteto ameacha mke ambaye ni Mama Monica Chiteto na wana watoto sita.

 

  1. Taratibu za kusafirisha mwili kuelekea Mpwapwa zinafanyika na mazishi yatafanyika siku ya tarehe 7 Septemba, Kanisa linatoa pole kwa familia ya Baba Askofu Chiteto, mkewe na watoto, wahudumu na Wakristo wote wa Dayosisi ya Mpwapwa na Kanisa lote kwa ujumla.

 

  1. Raha ya Milele umjalie Ee Bwana, na Mwanga wa Daima umwangazie. Roho ya  Baba Askofu GEORGE YORAM CHITETO na roho zao wote waaminifu walioitwa katika haki zipumzike kwa Amani. Amin.

The Most. Rev. Maimbo William Mndolwa,

ASKOFU MKUU, KANISA ANGLIKANA TANZANIA