“lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo.”
— 1 Petro 5:2

Mkutano wa Wachungaji wote wa Kanisa la Kiinjili la Kilitutheri Tanzania umefunguliwa Leo tarehe 11/09/2022 Jijini Dodoma katika Ibada iliyofanyika Usharika wa Kanisa Kuu Dodoma Mjini.
Akifungua Mkutano huo wa tano kwa niaba ya Mkuu wa KKKT. Askofu Dkt Frederick Shoo, Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt Alex Malasusa ameiomba serikali kuwasaidia viongozi wa dini kudhibiti suala la vijana kutopenda kufanya kazi badala yake kupenda zaidi kucheza michezo ya kubahatisha. Aidha Askofu Dkt Malasusa amesema kwamba Kanisa linakabiliwa na changamoto ya mafundisho ya uongo walimu wa uongo na mapato ya hila yanayotumia jina la Yesu. Mgeni Rasmi katika Ibada hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma MHE. ROSEMARY SENYAMULE ambapo amesema kuwa hali ambayo imeibuka kwa siku za hivi karibuni ya watu hasa wenye mahusiano ya karibu kuuana ni changamoto kubwa ambayo inaikabili jamii kwa sasa.
Amewaomba viongozi wa dini kuwasaidia katika hili kwani linasababishwa na kukosekana kwa hofu ya Mungu. Katika mkutano huu Wachungaji watajadili mada mbalimbali zikiwamo umoja na utambulisho wa Kanisa na Katiba moja ya KKKT.