Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mhashamu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewataka vijana wa KKKT-DKMs kugeuza mitandao ya kijamii kuwa fursa kwa kuitumia vema   kupata maarifa na uzoefu katika nyanja mbalimbali na kujiepusha na matumizi yasiyofaa.

 Askofu Dkt. Msafiri Mbilu ametoa wito huo kwenye ufunguzi wa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa idara ya vijana  KKKT-DKMs l tarehe: 19/12/2022 na kuendelea kuwasihi  vijana hao kujiepusha na mafundisho potofu yasiyo endana na msingi wa neno la Mungu.

Mafunzo haya yanafanyika katika Chuo cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) kilichopo Magamba Lushoto-Tanga na kinachomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Inaelezwa kuwa Dunia inakwenda kasi, na teknolojia inazidi kuimarika watu wanahabarika kupitia mitandao ya kijamii. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zinazofanya vizuri katika matumizi ya mitandao ya kijamii. Na hii inachagizwa na ongezeko la watumiaji wa simu janja na huduma ya mtandao (intaneti) nchini.

Mitandao hii si tu majukwaa ya kimawasiliano, bali ni fursa katika ulimwengu wa leo ya kukuza uchumi wa mtu mmo­ja mmoja na nchi kwa ujumla endapo itatumika vizuri. Licha ya kuwa na idadi kub­wa ya watumiaji wa huduma za intaneti na simu janja, lakini matumizi ya mitandao ya kijamii yameendelea kuwa kitendawili kwa Watanzania wengi.

Wapo ambao wamekuwa wakiitumia mitandao hiyo kwa namna sahihi ambayo imekuwa ikiwanufaisha kama vile kibiashara, kikazi na kie­limu na wale ambao wameku­wa wakiitumia ndivyo sivyo.

Katika miaka ya hivi karibu­ni, kumeshuhudiwa kukithiri kwa matukio ya upotoshwaji wa taarifa, usambazaji wa maudhui yasiyo na maadili (picha na video za utupu na lugha za matusi) na udhalilish­aji yanayofanywa mitandaoni.Hii inaashiria kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na kuwepo kwa kundi kubwa la Watanza­nia ambao hawajui kutumia mitandao hiyo kwa malengo ya kunufaika.

Ikumbukwe kuwa matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii yana athari kubwa kwa ustawi wa jamii ya sasa na hata baadaye kwa kuwa maud­hui yanayopandishwa katika majukwaa hayo yanadumu vizazi kwa vizazi.