
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amemshukuru Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa pamoja na Halmashauri Kuu ya KKKT kwa kuja na mpango wa pamoja kwa Dayosisi zote 28 za KKKT kuchangia kulipa deni linaloikabili KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs).
Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo kwenye Ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Jimbo la Kaskazini Usharika wa Nywelo na kusema kuwa mpango huo wa Dayosisi zote za KKKT wa kuisadia KKKT-DKMs ulikuwa ni moja ya agenda iliyojadiliwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya KKKT kilichofanyika Jijini Arusha hivi karibuni,ambapo pia kilihudhuriwa na Maaskofu wa Dayosisi zote 28 za KKKT pamoja na Makatibu wakuu.
Sambamba na hayo Dayosisi hizo zimefikia makubaliano hayo kwa lengo la kuzinusuru mali za Dayosisi ya Kaskazini Mashariki zisipigwe mnada huku akiwataka wana KKKT-DKMs kuongeza juhudi katika kuchangia kulipa deni la Dayosisi.
Aidha Ibada hiyo ilikuwa na matendo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzinduliwa kwa Usharika wa Nywelo na tendo la kuwabariki Vijana wa Kipaimara 68 huku watatu kati yao wakibatizwa ambapo walitoa kiasi cha Tsh 350,000 kwaajili ya kuchangia kulipa deni la Dayosisi baada ya kuungwa mkono na wazazi pamoja na wadhamini wao kilikusanywa kiasi cha Tsh 1,255,000.
Kuzinduliwa kwa Usharika huo wa Nywelo kunafikisha idadi ya Sharika za KKKT-DKMs kufikia 76 hadi hivi sasa.
