Msaidizi wa Askofu KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mchungaji Michael Mlondakweli Kanju, amewataka Wakristo kujenga moyo wa kujitoa kwa mali,sadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwani ipo siri kubwa ya kufanikiwa kwa kujitoa katika kumtumikia Mungu.
 
Msaidizi wa Askofu Mch. Michael Kanju ameyasema hayo leo tarehe 09/08/2024 kwenye makabidhiano ya nyumba ya familia namba 20 iliyoko kijiji cha Bungoi, kata ya Mlalo- Lushoto ambayo imetolewa na familia ya marehemu Mzee Saguti kwa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.
 
Kwa upande wake Mtoto wa Marehemu Mzee Saguti Dkt. Grace Saguti Jengo ambaye alikabidhi nyumba hiyo kwa niaba ya wanafamilia alisema kuwa wameona ni vema kutoa nyumba hiyo kwa Kanisa ikiwa ni alama na sadaka yao kwa Mungu na wamezingatia taratibu zote za makabidhiano ikiwemo hati ya makabidhiano na taratibu zote za kisheria zimefuatwa huku akiwataka Wakristo na watu wote kujenga moyo wa kujitoa.
 
Makabidhiano ya nyumba hii yameambatana na vitu vyote (samani) vilivyomo katika nyumba hiyo.