Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.

Ufunuo 14:13

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, leo tarehe 16/04/2022 akiwa katika Usharika wa Mlalo Jimbo la Kaskazini ameongoza Ibada ya mazishi ya Balozi Fanuel Ismail Kuzilwa.

 

Balozi Fanuel  Kuzilwa aliyezaliwa tarehe 21/07/1945 ameitwa mbinguni tarehe 12/04/2022, akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

KATIKA UTUMISHI: Marehemu Balozi Kuzilwa  katika uhai wake aliwahi kushika nafasi mbalimbali za kiuongozi, aliwahi kuwa Afisa Mwandamizi- Ubalozi wa Tanzania Nchini Angola na Nigeria.KATIKA TEUZI ZA RAIS aliteuliwa kuwa – Mkurugenzi wa Idara ya Africa, Wizara ya Mambo ya nje,Mnikulu, Balozi.Hata hivyo uongozi wa KKKT-DKMs utaendelea kumkumbuka Marehemu Balozi Kuzilwa kwa juhudi zake katika kuhakikisha Chuo Kikuu cha SEKOMU kinafunguliwa.

Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, unatoa pole kwa Familia ya Marehemu Balozi Fanuel Kuzilwa, ndugu jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu mzito. Mungu awape nguvu na faraja ya kweli katika kipindi hiki kigumu. BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe.

Naye atafuta kila chozi katika macho yao,wala mauti haitakuwepo tena,wala kilio,wala maumivu hayatakuwepo tena, kwa kuwa mambo ya kwanza , yamekwisha kupita UFUNUO 21:4.

Msaidizi wa Askofu   KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch. Michael Mlondakweli Kanju leo tarehe 14/04/2022 ameongoza Ibada ya mazishi ya Marehemu Mzee Nicholas Fredrick Mkala ambaye pia ni kaka wa Mch. Lewis Fredrick Shemkala wa  KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Usharika wa Hale.

Ibada imefanyika katika Kitongoji cha Kwamongo,Kijiji cha Kihitu,Kata ya Vuga Jimbo la Bumbuli,Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga. Marehemu Mzee Nicholas Fredrick Mkala aliitwa mbinguni Jumatatu  ya tarehe 11/04/2022   katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alikuwa anapatiwa matibabu.

Kwa niaba ya Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,kupitia kwa  msaidizi wa Askofu Mch. Michael  Kanju ambaye alimuwakilisha Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,Mch Dkt Msafiri Mbilu kwenye Ibada hiyo ya mazishi amesema kuwa, Uongozi unatoa pole kwa Familia ya Marehemu, ndugu jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huo mzito. Mungu awape nguvu na faraja ya kweli katika kipindi hiki kigumu. BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe.

 

 

 

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amechukuwa hatua ya kuwaandikia barua washarika waliopo ndani ya Dayosisi juu ya ombi la mchango kwaajili ya kukabiliana na deni la Dayosisi.

Akizungumza leo tarehe 10/04/2022 katika Ibada ya Jumapili iliyo ambatana na uzinduzi wa uchangiaji wa deni hilo katika Usharika wa Kana Tanga, amewashukuru wana Dayosisi kwa jinsi wanavyojitoa katika kumtumikia Mungu na kujitoa kwao kwa hali na mali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili Dayosisi.

 

Mkuu wa Jimbo la Pwani, Mch. Thadeus A. Ketto

Askofu Dkt. Mbilu anachukua hatua hii kutokana na Dayosisi kudaiwa madeni makubwa na miongoni mwa madeni hayo ni hatarishi sana kwani yanaweza kusababisha mali za Dayosisi mfano Majengo, Mashamba, Magari nk. kupigwa mnada ili kufidia gharama za wale wanaoidai Dayosisi. Ofisi ya Katibu Mkuu imeanza kupokea taarifa za awali juu ya hatua hizo juu ya mali za Dayosisi kupigwa mnada.

Mkurugenzi wa fedha na Utawala KKKT-DKMs CPA. PETER JOHN SINGANI

Kwa ujumla deni la Dayosisi lililorithiwa toka Uongozi uliopita ni takribani Tsh. 7,000,000,000 (Bilioni Saba) likiwepo deni la mkopo wa CRDB, Mishahara na stahiki za watumishi wengine katika vituo mbalimbali vya Dayosisi kama vile Ofisi Kuu, SEKOMU, pamoja na madeni ya Mifuko ya kijamii kama vile NSSF, PSSSF pamoja na kodi mbalimbali.

Kwa kupitia sadaka ya maendeleo ya KKKT-DKMs imeendelea kupunguza baadhi ya madeni hayo kama vile deni la CRDB na sasa limeshuka kutoka Tsh. 1,200,000,000 (Bilioni Moja na nukta 2) hadi kufika Tsh.792,000,000 (Milioni Mia saba na Tisini na Mbili). Na hapa Askofu Dkt. Mbilu anamshukuru Mkuu wa Jimbo la Pwani Mch. Thadeus A. Ketto, Washarika wa Kana na wana Dayosisi kwa ujumla   kwa jinsi wanavyoendelea kujitoa katika utoaji wa sadaka hiyo.

Hata hivyo ili kuweza kukabiliana na madeni hayo makubwa, Askofu Dkt. Mbilu analeta ombi kwa washarika kwani wao ni kiungo muhimu cha Dayosisi hii kuchangia deni hilo kama viwango vilivyo ainishwa kwenye barua walizo pokea kwa kadri Bwana atakavyowajalia. Na hapa anawaomba wana Dayosisi katika awamu hii ya kwanza kuanza kuchangia sehemu ya deni hilo katika kipindi cha miezi sita yaani kuanzia tarehe 01/04 hadi tarehe 31/10/ 2022.

Ili kuweza kuhakikisha kuwa fedha hizi zinafika mahali sahihi, kwa wana Dayosisi waliopo ndani ya Dayosisi wanaombwa kuingiza fedha hizo moja kwa moja kwenye akaunti ya Dayosisi ambayo ni: -

  • NMB HARAMBEE ACCOUNT No. 41610027028 au
  • CRDB ELCT NORTH EASTERN DIOCESE Acc.No.01J1029661501

Askofu Dkt. Mbilu ametanabaisha kuwa hatua ya pili ya uchangiaji kwa wadau wa maendeleo na wana KKKT-DKMs waliopo nje ya Dayosisi utatangazwa hivi karibuni. Uongozi unakutakia baraka za Mungu katika Utumishi wako shambani mwa Bwana.

 

 

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF) Mch. Anne Burghardt katika Ofisi za Makao Makuu ya KKKT (Arusha) ambapo Katibu Mkuu huyo yupo Nchini Tanzania kwa ziara ya Kikazi katika Kanisa la KKKT.

Aidha, Askofu Dkt. Mbilu ni mmoja kati ya wanakamati ya Ibada na Muziki ya Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF) inayoandaa  Mkutano Mkuu utakaofanyika Nchini Poland mwakani

Kamati hii iliundwa mwaka 2021 na ofisi ya Katibu Mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani ambayo makao Makuu yake yapo Geneva Uswis. Kamati hii ina wajumbe kumi kutoka Ujerumani,Canada,Norway,Hungary,Poland,Hong Kong,USA,Brazil,Switzeland na Africa ambapo mjumbe muwakilishi ni Askofu Dkt. Msafiri Mbilu.