Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewataka waumini kuishi maisha yanayofaa na kumpendeza Mungu katika ulimwengu huu na kuacha mambo yasiyofaa  ili kuwa na mwisho mwema. Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo kwenye Ibada  ya mazishi ya marehemu  Mch. Sabina Lumwe  na kusema kuwa marehemu Mch. Sabina lumwe alisimama vyema katika utumishi wake.

Akihubiri katika Ibada iliyofanyika Kanisa Kuu Lushoto leo tarehe 10/01/2023 Askofu Dkt. Mbilu, ameongeza kuwa, marehemu Mch. Sabina lumwe hakukengeuka na alisimama  katika utumishi wake kwa kufundisha mafundisho sahihi ya neno la Mungu hadi alipoitwa mbinguni.Hata hivyo Askofu Dkt.  Mbilu ameongeza kuwa KKK-DKMs itaendelea kuuenzi mchango mkubwa wa marehemu Mch.Sabina  lumwe alioutoa katika Kanisa.

Pia Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito kwa viongozi wa serikali ambao wamehudhuria katika Ibada hiyo akiwemo Mbunge wa Korogwe Vijijini kukazia juu ya uboreshwaji wa sheria za usalama barabarani  ili kuepusha ajali zinazojitokeza mara kwa mara ambazo zinatoa uhai wa watu wengi.

Askofu Mstaafu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Joseph Jali akitoa salamu zake kwenye Ibada hiyo ya mazishi ametoa pole kwa ndugu,jamaa na waombolezaji wote kwa ujumla kipekee kwa Askofu wa KKKT-DKMs Dkt. Msafiri Mbilu kwa kuondokewa na mmoja wa mtumishi wake aliyelitumikia Kanisa la Mungu kwa uaminifu na kuongeza kuwa marehemu Mch. Sabina Lumwe alikuwa mtu wa kuwajali, kuwapenda, kuwahudumia wengine na kupitia msiba wa Marehemu Mch. Sabina Lumwe iwe chachu ya kutumwa kwa upya katika kukaza yale bwana aliyowaitia kwa kila mmoja kwa kadri ya kipawa alichopewa na Mungu katika kulitumikia Kanisa la Mungu duniani kote.


Kwa upande wake Mbunge , Jimbo la Korogwe Vijijini, Mhe. Timotheo Mzava kwa niaba ya serikali ametoa pole kwa wafiwa wote huku akisema amepokea ushauri wa Baba Askofu Dkt.Mbilu kupeleka bungeni mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho ya sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara.

 Marehemu Mch. Sabina Lumwe alikua mwanamke wa kwanza kutoka KKKT-DKMs kwenda kusomea theolojia  katika Chuo cha Uchungaji Makumira hadi mauti inamkuta alikuwa  mchungaji mstaafu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambapo alitumika katika Sharika na vituo mbalimbambali na aliitwa mbinguni tarehe 08/01/2023 akiwa nyumbani kwake Lushoto.Uongozi wa KKKT-DKMs unaendelea kutoa pole kwa familia ya Marehemu, wana KKKT-DKMs ndugu, jamaa na marafiki popote pale walipo. BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na lihimidiwe.