
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amewataka wanafunzi wa Chuo cha Biblia Vuga kuendelea kufuata mafundisho yenye mafafanuzi sahihi wanayoyapata Chuoni hapo yanayozingatia taratibu na misingi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo tarehe 20/11/2023 akiwa kwenye ziara yake ya kikazi katika Chuo hicho huku akiwasihi wanafunzi hao kuacha kuiga mambo kutoka kwenye mitandao ya kijamii ambayo kwa sehemu yamekuwa yakikinzana na taratibu za Kanisa la KKKT.

Ameweka wazi kuwa mafundisho potofu ya neno la Mungu yamekuwa chanzo cha kuwachanganya Washarika hivyo kuwataka wanafunzi hao kutoka Dayosisi 6 za KKKT waliopo katika Chuo hicho kinachomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kutumia muda vizuri kujifunza Neno la Mungu kwa usahihi wake.
.

Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, aliambatana na msaidizi wake Mch. Michael Mlondakweli Kanju, kwenye ziara hiyo iliyokuwa na lengo la kukagua utendaji kazi,taaluma na maendeleo ya miradi Chuoni hapo.

