Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amefanya Ziara ya kikazi nchini Philippines, kuanzia tarehe 15/5/2024 hadi tarehe 05/06/2024, Ziara hii iliyowezeshwa na chama Cha kiinjili Cha kimisioni, United Evangelical Mission (UEM) imekuwa na malengo ya kumuwezesha Baba Askofu kuhudhuria Makongamano mbalimbali ya Kimisioni katika Chuo Kikuu cha Silliman kilichopo katika Jiji la Dumaguete Mkoa wa Negros Oriental.

Kongamano la Kimisioni lililoongozwa na Katibu Mkuu wa UEM Mch. Dkt Andar Parlindungan lilikaza juu ya Mtazamo wa Kisasa juu ya Huduma na Misioni na Jinsi UEM kama Chama cha Misioni kinavyojikita katika kutekeleza majukumu yake ndani ya Mtazamo wa Kisasa wenye mabadiliko mengi. Kongamano hili lilihudhuriwa na Wanafunzi wa Kitivo cha Theologia (Divinity School) cha Chuo Kikuu cha Silliman pamoja na Wahadhiri wa Kitivo hiki.

Katibu Mkuu wa UEM Dr. Andar akihutubia

Baba Askofu alipata nafasi ya kuwa na mazungumzo na Dean wa Kitivo cha Theologia Mch. Dkt. Van Cliburn M. Tibus na Wahadhiri wa Kitivo hiki pia alipata nafasi pia ya kuwa na mazungumzo na Rais wa Chuo Kikuu cha Silliman Dkt. Betty Cernol McCann.

Itakumbukwa kuwa Baba Askofu Dkt. Mbilu ambaye kabla ya kuchaguliwa kuwa Askofu wa KKKT-DKMS alikuwa Mhadhili Mwandamizi katika Chuo Kikuu hiki na alipata nafasi katika ziara hii kuagwa rasmi na Wahadhiri wenzake na Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu cha Silliman hususani Kitivo cha Theologia.

Vilevile Baba Askofu alipata nafasi  ya kuhudhuria Mahafali ya 111 ya Chuo hiki ambapo miongoni mwa Wanafunzi aliowafundisha walikuwa Wakihitimu Shahada ya kwanza na ya Pili.

Halikadhalika katika Mahafali hii Mtoto wa pili wa Baba Askofu, Joseph Msafiri Mbilu amehitimu Masomo yake ya Shahada ya kwanza ya Uhandisi (Bachelor of Science in Mechanical Engineering). Joseph aliipeperusha Bendera ya Tanzania nchini Philippines kwa kupewa tuzo ya Wanafunzi Watatu Bora wa Kimataifa nchini Philippines (Three Most Outstanding Students in the Philippines) tuzo inayotolewa na taasisi ya Philippine International Friendship and Understanding Association (PIFUA).

Katika ziara hii Baba Askofu Dkt. Mbilu alipata muda wa kukutana na Wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) wanaotokea KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, ambao ni Mch. Nuru Mwakapusya na Mch. Peter Bendera, Wanafunzi hawa wanafanya vizuri sana kwenye masomo yao na familia zao zinaendelea vizuri kuzoea maisha na utamaduni wa Kifilipino.

Chuo Kikuu cha Silliman ni miongoni mwa Vyuo bora na vyenye sifa kubwa katika Bara la Asia. Chuo hiki chenye wanafunzi kutoka Mataifa 59 Ulimwenguni pote kina jumla ya vitivo 19.Kilianzishwa mwaka 1901. Katika Chuo hiki watoto mbalimbali wa Viongozi na Watumishi wa UEM wamesoma shahada zao mbalimbali akiwepo Sandrine Kabango, Victor Polisi Kivava, Ajuna Fidon Mwombeki, Ninsiima Fidon Mwombeki, Joseph Msafiri Mbilu, Stephen Joseph  Rweyemamu, Miriam Josephat Rweyemamu, Jackson Msafiri Mbilu na wengine wengi.

Baba Askofu Dkt. Mbilu, akiwa na Wanafunzi aliowafundisha wa Divinity School waliohitimu wakiwa wamevalishwa Stola kama alama ya kazi yao ya Kikuhani.

Katika picha. Baba Askofu pamoja na Mama Wakiwa na familia ya Mchungaji Peter Bendera.

 

Bishop Erme Camba  miongoni mwa waanzilishi wa UEM.

 

Askofu Dkt. Mbilu baada ya kukabidhiwa cheti (Leadership Award for Being a President of the Overseas students fellowship) kwa niaba ya Jackson Mbilu ambaye hakuwepo kwenye Graduation.

 

Rais wa Chuo Kikuu cha Silliman Dkt. Betty Cernol McCann (wa pili kutoka kushoto)

Dean wa Divinity School Rev. Dr. Van Cliburn M. Tibus