Usharika  Mpya wa Bethania ni Usharika uliozaliwa kutoka katika Usharika Mama wa Kange. Usharika huu uliopo katika Jimbo la Pwani unaundwa na Mitaa miwili ambayo ni Mtaa wa SENTA pamoja na Mtaa wa PENUEL. Mtaa wa Senta upo katika maeneo ya Kange kasera karibu na Chuo cha Utumishi wa Umma na Mtaa wa Penuel upo katika maeneo ya Kasera. Mitaa yote hii miwili ilikua chini ya uangalizi wa Usharika mama wa Kange.

Mnamo Tarehe. 01/01/2022 Usharika mama wa Kange uliokuwa na Mitaa minne ( Kange Senta, Bethania,Penuel na Maweni) Uligawanywa rasmi na kupatikana Sharika Mbili ambazo ni Usharika wa Kange wenye Mtaa wa Senta pamoja na Mtaa wa Maweni  na Usharika mpya  Mteule wa BETHANIA wenye Mtaa wa Senta na Mtaa wa Penuel. Kwa sasa uliokuwa Usharika Mteule wa Bethania Umetimiza Miaka 2 na miezi sita hadi  kufunguliwa kwake Rasmi Ukiwa chini ya Uongozi wa Mchungaji GIBSON AGGREY.

UANZISHWAJI WA MTAA WA BETHANIA AMBAO NDIO SENTAYA USHARIKA

Mnamo mwaka 2005 Wakristo wa Kange Ufundi walikuwa wanasali Ibada ya Nyumba kwa Nyumba wakijumuika na Wakristo wa T.A.G kutokana na uchache wa waumini wa Kilutheri. Mnamo mwaka 2006 idadi ya Wakristo iliongezeka na wakaanzisha Ibada ya Nyumba kwa Nyumba. Tarehe 09.02.2006 Ibada ilifanyika kwa mara ya kwanza kwa Msharika aitwaye Tuomba Mbwambo ambapo Mchungaji Godfrey Walalaze (Mchungaji wa Usharika wa Kisosora wakati huo) alihudhuria katika Ibada hiyo.

Wakristo waliohudhuria Ibada hiyo ya kwanza ya jumuia ni; Mzee Alan Mnzava (Mzee wa Kanisa na familia yake), Mzee C. Msocha , Mzee Angelina Kangero, Mama Christina Mputa pamoja na Mama Vaileth Muna.Kupitia Ibada hiyo ya kwanza ya Jumuia, ndipo wazo la kupata  sehemu ya muda ya kuabudia lilizaliwa na lengo ni kuondoa changamoto ya umbali wa mahali pakuabudia hasa kwa Watoto kwani Wakristo hawa wote walikuwa wakisali katika Usharika wa Kisosora.

Mkristo mmoja wapo aliyekuwa katika Ibada hiyo (Mama Christina Mputa) alitoa taarifa Kwa Mch. Godfrey Walalaze kua kuna eneno la kiwanja cha Shule ya Chekechea (awali) ambacho kilikuwa wazi wakati huo  hivyo Kanisa linaweza kufuatilia ili kuanza jengo la Shule ya awali. Wazo hilo lilifanyiwa kazi na hatimaye eneo la Kanisa  ndipo majengo ya Shule ya awali yalipo na Ibada zinaendele  hadi leo hii katika madarasa hayo.

Kabla ya kupatikana kwa eneo hillo, Wakristo waliomba kuabudu katika madarasa  ya Chuo cha ualimu Kange (wakati huo), na mnamo tar. 30/04/2006 Mchungaji Godfrey Walalaze alizindua Mtaa mpya na kuuita “BETHANIA” jina ambalo hadi sasa ndio linalotumika.

VIONGOZI WA IDARA/KAMATI PAMOJA NA WAZEE WALIOCHAGULIWA WAKATI HUO

Badaa ya Kuanzishwa Rasmi kwa Mtaa wa Bethania, Wazee wa Kanisa pamoja na Viongozi mbalimbali wa idara walichaguliwa. Ifuatayo ni orodha ya wazee wa Kanisa waliochaguli pamoja na viongozi mbalimbali wa idara na Kamati. Wazee wa Kanisa waliohudumu wakati huo ni; Mzee Alan Mzava, Mama Maria Singano na Mama Elizabeth Shemela ambaye kwa sasa ni marehemu.

Uongozi wa Idara ya Jinsia na Watoto( Wanawake) ; Mama E. Lukumay (Mwenyekiti) ambaye kwa sasa ni marehemu, Mama Christina Mputa (Makamu Mwenyekiti), Mama E. Jeremia (Katibu), Mama Vaileth Muna (Katibu Msaidizi) na Mama Mary Kibwana (Mhazini). Waalimu wa Shule ya Jumapili;  mama Edna Greyson, Elisia Kimaro, Haneli Mnzava pamoja na Suzan Njana.

Kamati ya Ujenzi; Mzee Joshua Kimaro (Mwenyekiti) ,Mzee Singano (Katibu), Mama Mary Kibwana (Mweka Hazina),  Mama Christina Mputa, Mzee Alan Mnzava, Mzee Shemela Mzee Tulo Msakula, Mzee F. Mmbaga pamoja na  Mzee Fabian Njana.Kupitia kamati hii ya Ujenzi wakishirikiana na Wakristo wote wa Bethania kwa umoja wao  waliweza kujenga madarasa ya Chekechea ambayo ndiyo yanayotumika hadi sasa kuwa sehemu ya kuabudia kwa wakristo wote.Mnamo Mwaka 2009 Mtaa wa Bethania uliahamishiwa Usharika wa Kange kutoka usharika wa Kisosora na hii ni mara  baada ya Kange kuwa Usharika kamili.

WAATUMISHI MBALI MBALI WALIOHUDUMU BETHANIA

Usharika huu umepitia vipindi mbali mbali vya Uongozi wa Wachungaji, Mashemasi pamoja na Waijilisti. Watumishi wote hawa walitoa mchango wao mkubwa kwa maendeleo ya Usharika wa Bethania na Mitaa yake yote miwili.  Ifuatayo ni orodha ya Watumishi waliowahi kuhudumu BETHANIA katika vipindi mbalimbali;

  • Wachunguji waliohudumu wakati Mtaa wa Bethani ukiwa chini ya Usharika wa kisosora

Mchg. Godfrey Walalaze           2006-2007

Mchg. Joyce Temu                     2007-2008

Mchg. Kihiyo                   2008 miezi sita (6)

Mchg. Warehema Chamshama 2008-2009

  • Wachungaji waliohudumu wakati Mtaa wa Bethania ukiwa chini ya usharika wa Kange

Mch. Neema kamandu   2009-2012

Mch. Msafiri Joseph Mbilu 2013 miezi mitatu tu (Ambaye kwa sasa ni Askofu)

Mch. John Ndimbo 2012 (Mchungaji msaidizi)

Mch. Ngotonyingi  2012-2016

Mch. D. Ketho 2017-2021

Mch. Emmanuel Mtoi 2021-2022

Mch. Gibson Agrey  (Mchungaji masidizi na Mchungaji mwenza Usharika wa kange)

Wapo pia Waijilisti waliowahi kuhudumu wakati ukiwa bado ni Mtaa wa Betania pamoja na Penuel. Ifuatayo ni orodha ya Wainjilisti waliohudumu; Mwnj.Marko Ngongomi, Mwnj.Zayumba ,Mwnj.Neema shekilango, Mwnj.Neema Mgonja, Mwnj. Judice Sheiza, Mwnj.Joel Bendera, Mwnj.Charles Mngano, Mwnj. Rahel Shekinyashi Wainjilisti walio tumika wakati Ukiwa Usharika Mteule; Mwnj.Charles Mngano, Mwnj.Steven Bahati.  Mwnj.Furahini Dafwilo na Mwnj.Joshua Shekinyashi wanaendelea kutumika hadi sasa.

USHARIKA  MPYA WA BETHANIA.

Kupitia Kikao cha Halmashauri Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki chini ya Uongozi wa Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, walipoamua kusogeza huduma za Kichungaji karibu, Bethania ilipitishwa kuwa miongoni mwa sharika teule Katika Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.Mnamo tarehe. 01/01/2022 Usharika Mteule wa Bethania Uliazishwa Rasmi, na Mchungaji Gibson Aggrey aliyekuwa Mchungaji Mwenza katika Usharika wa Kange alipewa Jukumu la Kuanzisha Usharika wa Bethania wenye Mitaa miwili, Senta na Penuel.

Katika kipindi hicho Mchungaji Gibson Aggrey kwa Kushirikiana na Wazee wa Kanisa waliokuwepo na waliopo sasa, pamoja na Wakristo wote, walifanikiwa kuhakikisha malengo ya Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya kuanzisha Usharika na kupeleka huduma karibu yanatimia.