Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ameupongeza uongozi wa Taasisi ya Elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI), kwa kazi nzuri inayofanyika katika nyanja ya mafunzo kwa kuzingatia kasi na viwango katika utoaji wa Elimu katika taasisi hiyo inayomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa pongezi hizo leo tarehe 18/06/2024 akiwa katika taasisi hiyo iliyopo Magamba Lushoto akiwa kwenye ziara yake ya kukagua na kuona maendeleo ya Taasisi hiyo pamoja na na kupokea taarifa mbalimbali juu ya utendaji kazi na mambo yanayoendelea katika Taasisi hayo.

Hata hivyo baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya Taasisi hiyo Baba Askofu  Dkt. Mbilu,  ameutaka uongozi wa Taasisi hiyo kuendelea kubuni mbinu mbalimbali za kuitangaza Taasisi hiyo ili iendelee kufahamika na kuwafikiwa watu wengi huku akiweka wazi kuwa ufauru mzuri wa wanafunzi ni mojawapo ya vitu vitakavyo pelekea kuitangaza Taasisi hiyo ya Elimu ya KOTETI.

Pamoja na hayo Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu ameueleza uongozi wa Taasisi hiyo juu ya matamanio ya Uongozi  wa Dayosisi kuona siku moja Taasisi hiyo inasimama na kujiendesha yenyewe na kurudisha heshima ya kilichokuwa Chuo Kikuu cha SEKOMU kitu ambacho ni tamanio la watu wengi kuona siku moja heshima hiyo inarudi tena.

Kwa upande wake Kaimu  Mkuu wa Taasisi hiyo ya Elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI), Gerald Naphtaly Mng`ong`o ameeleza juu ya mipango ya uanzishwaji wa Idara nyingine za kitaaluma kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa kozi ya Maradhi ya Utamshi na Lugha (SLP), kwani uanzishwaji Idara ya  Maradhi ya utamshi na Lugha yaani  (Speech and Language Pathology) mpango wake unaendelea na hadi sasa umefikia  asilimia 50%.

Uwepo wa Mafunzo ya Ufundi (Vocational Studies) Taasisi hii inatarajia kufanya uratibu kwa kushirikiana na NACTVET na wadau wengine kuhakikisha UTC (Usambara Technical Center) inapata usajili rasmi wa VETA ili hadi kufika mwezi Aprili 2025 UTC iwe ni Idara kamili hasa katika fani za ;- Useremala, Ushonaji, Vyuma pamoja na Umeme.

Uwepo wa Idara ya Sayansi za Afya:  Kwa kuwa Taasisi ya KOTETI ina miundombinu ya kutosha kama madarasa, Ofisi na maabara; Taasisi ya Elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) inajipanga kuanzishe kada nyingine za Afya kama vile utabibu, Maabara na Usimamizi wa kumbukumbu za matibabu.

Hata hivyo Uongozi na Wanafunzi wa Taasisi ya Elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) wamemshukuru sana Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kwa kuwa mstari wa mbele kufuatilia na kusimamia maendeleo ya Taasisi hiyo ikiwemo uanzishwaji wa idara hizo. Ziara hii ya Baba Askofu imempa nafasi ya kuzijua zinazo ikabili Taasisi hiyo.

 

Moja ya changamoto iliyowasilishwa  kwa Baba Askofu ni uhaba wa Computer katika Taasisi hiyo ambapo  Baba Askofu ameanza kutatua changamoto hiyo kwa kufanikisha upatikanaji  Computer 10 mpya na za kisasa zitakabithiwa kwa Uongozi wa Taasisi hiyo hivi karibuni.