Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amewashukuru Washarikwa wa Usharika wa Mlalo na wana KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa namna wanavyojitoa katika kumtumikia Mungu.

 Askofu Dkt. Msafiri Mbilu, ameyasema hayo katika Ibada iliyofanyika leo jumapili tarehe 23/6/2024 katika Jimbo la Kaskazini Usharika wa Mlalo  iliyokuwa imeambatana na tendo la kuwabariki  vijana wa Kipaimara pamoja na ubatizo wa watu wazima  ambapo amewataka Wakristo kujitoa kwa moyo kwa vipawa mbalimbali walivyo barikiwa na Mungu  huku wakisimama katika kweli ya Mungu ili kweli hiyo siku moja iweze kuwapa nafasi ya kuurithi uzima wa milele.

 Kwa upande wao Vijana hao waliobarikiwa walimpongeza Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu, kwa jitihada zake za kusomesha Wanafunzi kutoka katika Sharika mbalimbali za KKKT-DKMs huku wakiwashukuru walimu na Wazazi waliowaongoza kwenye mafundisho yao huku  wakiongeza kuwa Wachungaji, Wainjilisti na walimu mbalimbali wamewajenga na kuwaasa katika nyanja mbalimbali za maisha kupitia mafundisho mbalimbali yaliyo yapata na kuahidi kuishi kama walivyo fundishwa.

 “Tunatambua jitihada zako pamoja na wasaidizi wako katika kusimamia mambo ya elimu na Afya japo kuna ukinzani mkubwa unaosababishwa na uwepo wa deni kubwa la Dayosisi, tunaona na kushuhudia kazi za maendeleo zikifanyika na tunaona kwa sasa Wanafunzi wanaosomeshwa na Sharika wamekuwa mlango wa kufanya Shule zetu ziendelee kuwa hai, mwaka huu wako kidato cha nne! Hongera sana Baba Askofu Mbilu” .Alisema mmoja wa Vijana hao waliobarikiwa.

 Aidha vijana hao wameongeza kwa kusema kuwa uwepo wa Chuo cha Kati cha (KOTETI) umeendelea kurudisha matumaini ya Chuo Kiku huku wakiamini kuwa  muda si mrefu Chuo Kikuu kitarejea kwani majengo yapo huku wakitoa pongezi kwa Baba Askofu Dkt Mbilu kwa ujenzi wa vibanda vya biashara katika eneo la Ofisi Kuu Lushoto sambamba na uanzishwaji wa mradi wa kilimo cha parachichi.Wakiwa na tumaini kuwa miradi hiyo itasaidia shughuli za uendeshaji wa Kanisa.

 Vile vile vijana hao wameunga mkono jitihada za ulipaji deni la Dayosisi, kwa kutoa  jumla ya shilingi Tsh. 390,000 na kuwaomba wazazi, walezi  na Washarika walioshiriki katika Ibada hiyo kuwaunga mkono kwa  kutoa kiasi chochote walicho nacho ili kuendelee kwezesha kulipa deni hilo la Dayosisi ambapo baada ya kuungwa mkono ilipatikana keshi ya Tsh. 610,000 ahadi Tsh. 166,000 na kufanya Jumla ya mchango wa Vijana hao kuwa Tsh.1,166,000.

 Vijana hao waliobarikiwa walianza  mafundisho mwaka 2022 wakiwa wavulana 46 na wasichana 24 Ambapo leo jumapili waliobarikiwa ni wavulana 51 na Wasichana  27 na kufanya  jumla kuwa 78 na watatu kati yao walibatizwa.