Waziri Ofisi ya Rais Uwekezaji na Mipango Mhe. Prof. Kitila Mkumbo,ameihamasisha Jumuiya ya Kikristo Tanzania ambayo inajulikana kwa kifupi (CCT) kujikita katika swala zima la Uwekezaji katika nyanja mbalimbali kama vile Kilimo Viwanda na Utalii kwani Serikali imefungua milango mingi ya Uwekezaji katika kipindi hiki.
Prof. Kitila Mkumbo ambaye ndiye aliyekuwa Mgeni Rasmi kwenye Mkutano huo wa 58 wa Halmashauri Kuu ya CCT uliofanyika tarehe 03/07/2024, katika Mkutano huo uliofanyika katika kituo kinachomilikiwa na CCT, cha Morogoro Women Training Center (MWTC).
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ni mmoja wa wajumbe walioshiriki katika mkutano huu,mbali na Baba Askofu Mkutano huu pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro mjini.

Jumuiya ya Kikristo Tanzania ambayo inajulikana kwa kifupi kama CCT (Christian Council of Tanzania), ni Taasisi ya Ki-ekumene inayowakilisha Umoja wa Madhehebu ya Kikristo ya Kiprotestanti. Kwa sasa CCT inaundwa na Makanisa mbalimbali Wanachama na Vyama vya Kikristo au vyenye mwelekeo wa kikanisa kutoka Tanzania Bara na Visiwani. Taasisi hii ilianzishwa rasmi tarehe 23 Januari, 1934 kutokana na maono ya Wamisionari kutoka Kanisa Anglikana, Kanisa la Moravian na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri. Wamisionari hawa walipata maono ya kujenga umoja kati ya makanisa wanachama ambao utajihusisha na masuala mbalimbali ya ki-imani, kimaendeleo na kijamii. Muungano huu ulijulikana kwa jina la Kiingereza, Tanganyika Missionary Council (TMC).


Mnamo mwaka 1964 Mungu aliwapa maono watumishi wake Baba Askofu Stephano Reuben Moshi (Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania), Baba Askofu Theofilo Kisanji (Kanisa la Moravian Tanzania) na Baba Askofu Mkuu John Sepeku (Kanisa Anglikana Tanzania) kubadilisha usajili wa TMC kuwa Christian Council of Tanzania (CCT), jina linalotumika hadi sasa. Idadi ya Makanisa yaliyopo chini ya CCT imekuwa ikiongezeka kutoka Makanisa matatu (3) ya mwanzo mwaka 1934 hadi kufikia makanisa ya Kiprotestanti kumi na mbili (12) yaliyopo mwaka 2021.


Kwa sehemu kubwa Makanisa Wanachama wa CCT yanafuata mapokeo ya Makanisa ya Kiinjili. Aidha, ili kuwezesha kukua na kuimarika kwa umoja wa kweli, Makanisa Wanachama yanatumia utaratibu unaofanana katika mambo muhimu. Mambo hayo ni pamoja na Ukiri wa Imani ya Mitume (Apostles Creed), Ukiri wa Imani ya Nikea (Nicene Creed) katika kuendeleza ufalme wa Mungu kwa njia ya mahubiri na kuunganishwa kuwa mwili mmoja katika Yesu Kristo.