Askofu wa KKKT- Dayosisi ya Kaskazin Mashariki, Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amesema watoto wanatakiwa kufundishwa kanuni za maisha ili waweze kujitegemea katika sekta mbalimbali na tena wafundishwe neno la Mungu nakuziishi amri kumi za Mungu.
Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo wakati akihubiri katika Ibada iliyofanyika tarehe 05/10/2024 akiwa katika Jimbo la Tambarare Usharika wa Kwalukonge ambapo ameongeza kuwa kwa sasa kumekua na mafundisho mengi potofu ambayo yanakuja kwa kasi sana hivyo wazazi pamoja na walezi wana jukukumu kubwa na kuhakikisha wanawafundisha watoto wao Neno la Mungu kwa usahihi ili wasiyumbishwe na mafundisho hayo potovu.
Katika Ibada hiyo jumla ya vijana 73 walibarikiwa na watatu kati yao walibatizwa ambapo pia waliunga juhudi za Askofu Dkt. Mbilu,katika kukabiliana na deni linaloikabiri Dayosisi kwa kuchangia kiasi cha shilingi 279,000/= na baadae kuungwa mkono na wazazi na walezi na kufikisha jumla ya shilingi 1,367,700/=
Sambamba na hilo,Askofu Dkt Mbilu alihamasisha mchango kwaajili ya ujenzi unaoendelea wa Kanisa la Kwalukonge na kiasi cha shilingi 560,200/= kilipatikana na ahadi kiasi cha shilingi 460,000/= ambayo imepelekea jumla ya shilingi 1,020,200/= kupatikana kwaajili ya ujenzi huo.