Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu,Tarehe: 12/11/2023, akiwa katika Jimbo la Kusini, Usharika wa Ubiri, ameongoza Ibada iliyokuwa na tendo la kuwabariki Vijana wa Kipaimara.
Ambapo jumla ya Vijana wapatao 29 wamebarikiwa na 3 kati yao wamebatizwa, wakisoma Risala yao mbele ya Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu vijana hao wamemshukuru Baba Askofu Dkt Msafiri Mbilu kwa kufika na kuungana nao katika siku ya kubarikiwa kwao na wamempongeza Baba Askofu kwa jitihada zake katika kuiongoza na kuiletea maendeleo Dayosisi.
Wameongeza kuwa wana tambua kazi kubwa inayofanywa na KKKT-DKMs katika kumhudumia mwanadamu kiroho, kimwili na kiakili hasa kazi kubwa inayofanyika katika kufufua na kuimarisha vituo vinavyotoa huduma kwa watu wenye mahitaji maalumu
.
Katika Ibada hiyo Vijana hao walitoa kiasi cha Tsh 90,000 kwaajili ya kuchangia ulipaji wa deni la Dayosisi, ambapo pia waliomba kuungwa mkono na wazazi,walezi pamoja na washarika walioshiriki katika Ibada hiyo na kufanikiwa kukusanya jumla ya Ths. 1,312,700/= ambapo fedha hizo zimeelekezwa katika kulipa deni la Dayosisi.
Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu,Tarehe: 11/11/2023, akiwa katika Jimbo la Kusini, Usharika wa Ambangulu, ameongoza Ibada iliyokuwa na tendo la kuwabariki Vijana wa Kipaimara.
Ambapo jumla ya Vijana wapatao 62 wamebarikiwa na wawili kati yao walibatizwa, wakisoma Risala yao kwa Baba Askofu Dkt Msafiri Mbilu, wameeleza kuwa moja ya mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka 2 katika darasa lao la Kipaimara ni pamoja na kuandaliwa vema kiimani.
Wameongeza kuwa ili kumshinda mwovu shetani na hila zake wataendelea kusimama katika Imani, kujifunza neno la Mungu kwa kulisoma na kutembea nalo katika maisha yao huku wakiitegemea neema ya Mungu katika kuyatenda mapenzi yake.
 
Katika Ibada hiyo Vijana hao walitoa kiasi cha Tsh 200,000 kwaajili ya kuchangia ulipaji wa deni la Dayosisi, ambapo pia waliomba kuungwa mkono na wazazi,walezi pamoja na washarika walioshiriki katika Ibada hiyo na kufanikiwa kukusanya jumla ya Ths. 1,198,000/= ambapo fedha hizo zimeelekezwa katika kulipa deni la Dayosisi.

Kuelekea kilele cha uchangiaji wa Tsh 30,000 kwa kila msharika wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki-(KKKT-DKMs) kwa ajili ya kupunguza deni linaloikabili Dayosisi kitakacho fanyika katika Jimbo la Tambarare Usharika wa Korogwe tarehe 17/12/2023. Askofu Dkt Msafiri Mbilu amewashukuru wale wote ambao wameingia kazini kuchangia deni hilo.

Askofu Dkt. Mbilu ameongeza kuwa siku hiyo itakuwa ni kilele cha kukusanya kiasi hicho na kupata taarifa za uchangiaji kwa kila Usharika “Awali ya yote napenda kuwashukuru ninyi wote kwa jinsi mlivyopokea wito huu wa kila mmoja kuchangia Tsh. 30,000/=. Fedha hizi zimesaidia sana kupunguza deni la Dayosisi. Ninapenda kuwajulisha kuwa tutakuwa na siku rasmi ya kilele cha mchango huu wa Tsh. 30,000 tarehe 17/12/2023 kwenye Jimbo la Tambarare Usharika wa Korogwe, wapo watu wengi waliomaliza na kuendelea kuongeza zaidi na zaidi patano la kuchangia kiasi cha Tsh.30,000, lakini pia wapo ambao wameanza lakini hawajakamilisha nawasihi kukamilisha patano letu".Alisema  Askofu Dkt. Mbilu.

Baba Askofu amesisitiza kwa wale wote ambao bado hawajakamilisha mchango wa Tsh. 30,000/= wanaombwa kukamilisha mchango wao kupitia Sharika zao ili siku ya kilele taarifa ya kila Usharika iwasilishwe bila deni, ili kutoa mwanga wa jinsi ya kujipanga na awamu nyingine za uchangiaji.

Kutokana na ukubwa wa deni la Dayosisi harambee hizi zitakuwa endelevu,Baba Askofu anazidi kuwatakia baraka za Mungu ninyi nyote kwa kujitoa kwenu ili kazi ya Mungu iendelee kusonga mbele kwani kwa mshikamano uliopo ipo siku deni hili litakwisha na kurudisha heshima ya Dayosisi yetu.

MATUKIO KATIKA PICHA TAREHE 02/11/2023:- Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu pamoja na kikundi cha Wadiakonia 30 kutoka Ujerumani ambao wameitembela Dayosisi yetu na wamepata nafasi ya kutembelea shule ya Msingi ya Irente Rainbow School inayomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.Baba Askofu amewashukuru wadiakonia hawa wenyeurafiki na shule hii kwa namna wanavyojitoa kwa hali na mali katika kuchangia maendeleo ya shule hiyo.Katika kuchangia maendeleo na kazi mbalimbali katika shule hiyo wadiakonia hawa wametoa kiasi cha Tsh: 7,891,200.