Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amesema katika uongozi wake ataendelea kutambua mchango na kazi kubwa iliyofanywa na Wachungaji, Mashemasi pamoja na watumishi wengine waliostaafu ambao  walioitumikia Dayosisi kwa nyakati tofauti na  kuongeza kuwa pamoja na kustaafu utumishi wao bado wanao mchango wa uzoefu , ujuzi na uwezo wa kushauri ili kuondoa makosa katika utendaji.

Askofu Dkt. Msafiri Mbilu ameyasema hayo tarehe 28.11.2023 kwenye ufunguzi wa kikao chake na Wachungaji pamoja na Mashemasi Wastaafu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki katika ukumbi wa mikutano wa Benjamin William  Mkapa Auditorium, uliopo katika, Taasisi ya Elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) Magamba Lushoto Tanga ambacho kitafanyika kwa siku mbili ambapo kitahitimishwa tarehe 29.11.2023.

Hata hivyo Askofu Dkt. Mbilu ameweka wazi kuwa wastaafu hao watapewa taarifa kutoka Kurugenzi ya Misioni na Uinjilisti,Kurugenzi ya Huduma za Jamii, Kurugenzi ya Uchumi na Mipango pamoja na Kurugenzi ya Fedha na Utawala ili wastaafu hao wapate nafasi ya kutoa maoni na ushauri wao.

Kwa upande wao Mch. Mstaafu Nkhanileka Chedi, Mch. Mstaafu Zawadiel Mkilindi pamoja na Mch. Mstaafu Yohana Mmaka wamesema wamefurahi kwa kupata nafasi ya kukumbukwa na Baba Askofu Dkt.Mbilu kama wastaafu nakuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuitumikia Dayosisi pamoja na kushauri juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Dayosisi.

Kikao hicho kitaangazia kazi za maendelo ikiwemo miradi mbalimbali inayotekelezwa na Dayosisi pamoja na kuwasilishwa kwa taarifa  ya maendeleo ya Shamba la Irente Farm, Taasisi ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) na Ujenzi wa vibanda vya biashara unaoendelea ndani ya Dayosisi.

MATUKIO KATIKA PICHA: Askofu wa KKKT -Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, Tarehe 25/11/2023 akiwa katika Jimbo la Tambarare Usharika wa Mtonga aliongoza Ibada iliyokuwa na tendo la kuwabariki Vijana wa Kipaimara,Ibada hiyo ilitanguliwa na ufunguzi wa nyumba ya mtumishi.

Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, unatoa pole kwa Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo Mkuu wa KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini,kufuatia kifo cha Askofu Mstaafu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Erasto Kweka, kilichotokea tarehe:25/11/2023.

Uongozi unatoa pole kwa familia, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Kaskazini ,Wakuu wa Majimbo wa Dayosisi ya Kaskazini, Wakuu wa Idara zote  za Dayosisi Wachungaji wote wa Dayosisi ya Kaskazini pamoja na  Washarika wote wa Dayosisi ya Kaskazini.

 BWANA ametoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe.

Askofu wa KKKT -Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, Tarehe 24 / 11 / 2023 ameanza ziara yake ya Kikazi Katika Jimbo la Tambarare Usharika wa Mtonga na kuongoza Ibada zilizokuwa na matendo mbalimbali ikiwemo uwekaji wa jiwe la ufungizi wa Kanisa Mtaa wa Ngua,Ibada ya kuweka jiwe la msingi la Kanisa Mtaa wa Tabora, Ibada ya kuwabariki Vijana wa Kipaimara katika Mtaa wa Sayuni na ufunguzi wa Kongamano la ITA NAE ATAITIKA linalofanyika katika Senta ya Usharika wa Mtonga.